22/05/2026
Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), Bw. Aristid Kanje, amewataka wataalamu wa usalama wa viwanja vya ndege kutumia maarifa waliyopata kuongeza ufanisi kazini. Amesisitiza kuwa wao ni nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa usafiri wa anga kwenye ukanda huu
Bw. Kanje ametoa wito huo leo Mei 22, 2026 wakati akifunga mafunzo ya Maafisa Usimamizi wa Usalama wa Viwanja vya Ndege (Airport Security Supervisors) yaliyoendeshwa yakiendeshwa chuoni hapo kuanzia tarehe 18 Mei 2026.
Alisema usalama wa viwanja vya ndege ni msingi muhimu wa sekta ya usafiri wa anga, hivyo wataalamu hao wanapaswa kufanya kazi kwa umakini mkubwa katika kubaini, kuzuia na kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa kutumia mbinu na maarifa ya kisasa waliyojifunza.
“Sekta ya usafiri wa anga inahitaji umakini wa hali ya juu. Nendeni mkatumie ujuzi mliojifunza kuimarisha usalama katika maeneo yenu ya kazi,” alisema Bw. Kanje.
Aidha, alibainisha kuwa chuo hicho kitaendelea kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa ili kuhakikisha wataalamu wa usalama wanakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya zinazoendelea kujitokeza duniani.
Kozi hiyo imehusisha washiriki 11 kutoka taasisi mbalimbali za usafiri wa anga, wakiwemo washiriki watatu kutoka Mamlaka ya usafiri wa anga ya Uganda, watatu kutoka Zanzibar Aviation Services & Travel (ZAT), watatu kutoka Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania (TAA) na wawili kutoka Mamlaka ya viwanja vya ndege ya Zanzibar na Pemba. Ushiriki huo umetajwa kusaidia kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu wa kiusalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mafunzo hayo ya siku tano yalifunguliwa rasmi Mei 18, 2026 na Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Bi. Angela Kabali.
Washiriki wote wametunukiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo baada ya kukamilisha ratiba yote ya mafunzo kwa mafanikio.
20/04/2026
Jumla ya washiriki 20 kutoka Tanzania, Uganda na Eswatini wanashiriki katika kozi ya Vihatarishi katika Usafiri wa Anga (Risk Management Course) inayotolewa na Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kwa niaba ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tano, tarehe 20 Aprili 2026, Mkuu wa Chuo cha CATC, Bw. Aristid Kanje, alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo katika kuimarisha usalama wa anga kikanda.
“ICAO imeweka viwango, nasi tunavitekeleza. Mafunzo haya ya Vihatarishi katika Usafiri wa Anga (Risk Management Course) ni hatua muhimu katika kujenga ukanda wa anga unaotegemewa,” alisema Bw. Kanje.
Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea washiriki uwezo wa kutambua, kuchambua na kudhibiti vihatarishi vya kiusalama katika sekta ya usafiri wa anga. Aidha, yanakusudia kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya usalama na kukuza ushirikiano wa kikanda.
Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka CATC, Bi. Christine Bgoya, alielezea kwa kina umuhimu wa mafunzo hayo, akibainisha kuwa yatawaongezea washiriki mbinu za kitaalamu za usimamizi wa vihatarishi. Pia alieleza kuwa mafunzo hayo yataboresha ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi shiriki, hali itakayochangia kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya usalama wa anga.
Kupitia mafunzo haya, Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kinaendelea kuonesha dhamira yake ya kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa, pamoja na kuchangia kikamilifu katika kuimarisha usalama, ufanisi na maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
02/04/2026
Jumla ya washiriki 37 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Uganda(UCAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Somalia(SCAA) na nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea (Conakry), ambazo zinajumuishwa katika Roberts Flight Information Region (Roberts FIR), wamehitimu mafunzo kozi nne tofauti yaliyolenga kuimarisha usalama na ufanisi wa sekta ya usafiri wa anga barani Afrika katika Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Salim Msangi, amefunga rasmi kozi hizo za Usimamizi wa Uongozaji Ndege katika hafla iliyofanyika Aprili 2, 2026 katika Makao Makuu ya TCAA, Ukonga–Banana, Dar es Salaam.
Akizungumza, katika hafla hiyo Bw. Msangi aliwapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na mafanikio waliyoonesha, na kutoa shukrani kwa mamlaka za anga za Somalia, Uganda, na Robert FIR kwa kushirikiana na CATC katika kuendeleza taaluma ya usafiri wa anga.
Bw. Msangi alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuwa kitovu cha mafunzo ya usafiri wa anga barani Afrika kutokana na uwekezaji katika miundombinu ya mafunzo na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Bw. Msangi pia aliwahimiza wahitimu kufuata taratibu za usalama, kufanya kazi kwa umakini, kudumisha mawasiliano sahihi, na kuweka usalama mbele katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha CATC, Bw. Aristid Kanje, alisema kuwa mafunzo haya yamejwajengea washiriki uwezo wa kitaaluma kwa wahitimu na kuwawezesha kutoa huduma ya udhibiti wa anga kwa usalama, kwa ufanisi na kwa weledi.
Mchanganuo wa kozi zilizohitimishwa ni pamoja na kozi ya ‘Basic Aerodrome Control’, iliyohusisha washiriki 21 kutoka SCAA, iliyoanza tarehe 13 Oktoba hadi 21 Novemba 2025; kozi ya ‘Aerodrome Control’, iliyohusisha washiriki 21 kutoka SCAA, iliyoanza tarehe 24 Novemba 2025 hadi 30 Januari 2026; kozi ya ‘Area Control Procedural’, iliyohusisha washiriki 21 kutoka SCAA, iliyoanza tarehe 2 Februari hadi 3 Aprili 2026; pamoja na kozi ya ‘Basic Aerodrome’, iliyohusisha washiriki 16 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Uganda (UCAA) na Roberts FIR, iliyoanza tarehe 23 Februari hadi 3 Aprili 2026.
01/04/2026
WATAALAMU NANE WAHITIMU MAFUNZO YA UMENEJA WA USALAMA WA USAFIRI WA ANGA CHUO CHA CATC KWA UFAULU WA JUU
Jumla ya watalaam nane wamehitimu kwa ufaulu wa juu kozi ya Mameneja wa Usalama wa Usafiri wa Anga (AVSEC Manager), katika Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), na kupewa pongezi kwa ufaulu huo wa kiwango cha juu.
Akizungumza mnamo Machi 31, 2026, wakati wa hafla ya kufunga kozi hiyo, Mkuu wa Chuo cha CATC Bw. Aristid Kanje alisema kozi hiyo iliyoanza Machi 23, 2026, imehitimishwa rasmi Machi 31, 2026, na kusisitiza kuwa ufaulu huo ni uthibitisho wa ubora wa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo. Aidha, aliwataka wahitimu kuendeleza viwango hivyo wanaporejea katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga(ICAO).
Bw. Kanje aliongeza kuwa matokeo hayo yanaakisi nidhamu, umakini na juhudi walizoonesha tangu kuanza mpaka kumalizika kwa mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Bi. Angela Kabali, amewapongeza wahitimu hao kwa juhudi zao na kuwataka kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kabali pia aliwahimiza wahitimu kushirikiana kwa karibu na wadau wengine wa sekta ya usafiri wa anga pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma hiyo ili kuimarisha usalama na ufanisi katika sekta hiyo muhimu.
Hafla ya kufunga kozi hiyo ilihitimishwa kwa utoaji wa vyeti kwa washiriki wote,ikiwa ni uthibitisho kuwa wamekidhi vigezo vya kitaaluma na kiutendaji vinavyohitajika katika usimamizi wa usalama wa anga kulingana na taratibu na kanuni za ICAO.
Miongoni mwa wataalamu hao nane ni kutoka taasisi mbalimbali, wakiwemo wawili kutoka Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania, mmoja kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, watatu kutoka Mamlaka ya Usafiri wa anga ya nchini Uganda, mmoja kutoka Jeshi la Wananchi la Uganda na mmoja kutoka Wakala wa Usimamizi wa Ulinzi na Usalama wa Usafiri wa Anga Africa Mashariki (CASSOA) iliyopo nchini Uganda.
Hatua hii inadhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda katika usalama wa anga.
24/02/2026
Washiriki 26 kutoka Malawi, Uganda na Liberia Wahudhuria Kozi CATC
Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) mnamo Februari 23, 2026, kimefungua rasmi mafunzo mawili tofauti yanayowakutanisha wataalamu wa sekta ya anga kutoka nchi za Malawi, Uganda na Liberia, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usalama na weledi katika usafiri wa anga.
Mafunzo hayo yanahusisha wanajeshi 10 kutoka nchini Malawi wanaohudhuria mafunzo ya siku tano ya Usafirishaji wa Bidhaa Hatarishi kwa Njia ya Anga, yanayolenga kuwajengea uwezo katika utambuzi, uainishaji, ufungashaji na usafirishaji salama wa bidhaa hatarishi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Wakati huo huo, wataalamu 16 wa huduma za Uongozaji Ndege 12 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Uganda (UCAA) na wanne kutoka Roberts Flight Information Region nchini Liberia wameanza mafunzo ya wiki sita ya mafunzo ya awali ya uongozaji ndege (Basic Aerodrome Control Course), yanayolenga kuimarisha umahiri katika udhibiti na uongozaji ndege katika mazingira ya uwanja wa ndege.
Akizungumza wakati wa ufunguzi mafuzo hayo, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi wa CATC, Bi Angela Kabali, alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama wa usafiri wa anga, yakilenga kukuza taaluma, uwajibikaji na ufanisi wa kiutendaji kwa washiriki.
Aliongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, washiriki watapata fursa ya kujifunza kwa vitendo na kubadilishana uzoefu kutoka nchi mbalimbali, jambo litakalosaidia kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kujenga mtandao wa kitaaluma miongoni mwa wataalamu wa anga barani Afrika.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yanaakisi dhamira ya CATC ya kuendelea kutoa mafunzo yenye ubora wa kimataifa, sambamba na kuchangia katika kuimarisha usalama, ufanisi na maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga katika ukanda na bara kwa ujumla.
22/01/2026
Menejimenti ya TCAA Yatembelea Mradi wa Ujenzi wa Majengo ya CATC
Menejimenti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Salim Msangi imetembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa majengo ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) uliopo eneo la Banana, jijini Dar es Salaam, Januari 21, 2026.
Lengo la ziara hiyo ni kujionea hatua za utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini. Pia ikiwa ni sehemu ya juhudi za uongozi wa mamlaka kufuatilia kwa karibu hatua za utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na serikali .
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Msangi alisema uongozi wa TCAA unaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kimataifa.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya chuo cha CATC kutakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza rasilimali watu wenye ujuzi wa kitaalamu katika sekta ya anga, sambamba na kupunguza utegemezi wa mafunzo ya nje ya nchi.
“Mradi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini. Tunahakikisha kuwa utekelezaji wake unazingatia ubora, ratiba na viwango vya kimataifa,” amesema Bw. Msangi.
Kwa upande wake, Meneja Mradi Mhandisi Stephen Mwakasasa alisema ujenzi unaendelea kulingana na michoro na usanifu uliokubaliwa, huku akibainisha kuwa usimamizi wa karibu unaendelea kufanyika ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa.
Ziara hiyo pia iliwezesha Menejimenti ya TCAA kupata maelezo ya kina kuhusu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, changamoto zilizopo pamoja na mikakati ya kuendelea kuboresha utekelezaji wa mradi huo hadi kukamilika kwake.
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga kunatarajiwa kuongeza uwezo wa taifa katika kutoa mafunzo ya kitaalamu ya anga na kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.