Mwalimu Makoba

Mwalimu Makoba

Share

Katika ukurasa huu, utapata mambo yote yahusuyo elimu, riwaya na mengine yasiyotajwa.

17/10/2022

Mzalendo Kizimbani
Sehemu ya 15

Sekondari alisoma mbali na nyumbani. Shule ya serikali iliyokuwa mkoa wa mbali na ilikuwa ya bweni. Mara moja Baba alipata taarifa kuwa Mako kaonekana mjini, akapiga simu shule, akaambiwa kijana yupo na anasoma kwa bidii.

Baada ya kumaliza kidato cha nne, kidato cha tano na sita hakikuchukua muda, alimaliza na kwenda kulitumikia jeshi la kujenga taifa kwa miezi mitatu. Baadae alianza chuo kikuu akisomea shahada ya elimu. Mara tano Baba alienda chuo kumtafuta ili amjulie hali, hakumkuta, lakini alipewa taarifa mwanafunzi huyo yupo ila huonekana muda wa vipindi na haishi katika eneo la chuo. Baba alipomuuliza Mako, akajibu anaishi eneo la chuo na huonekana hapo muda wote. Hata hivyo akasisitiza Baba anapotaka kuja kumtembelea atoe taarifa kwani hujificha sehemu kujisomea na kufanya iwe ngumu kuonekana na watu wengine.

Alimaliza chuo, akakaa nyumbani wiki moja halafu akasema amepata shule kufundisha. Jina la shule alilotaja Baba alilitafuta hakulipata. Mako alishakuwa mtu mzima, alimuacha na maisha yake.

Mako aliondoka nyumbani akisema anafundisha katika shule yake isiyofikika. Muda mwingi hakuonana na Baba lakini waliwasiliana. Hata hivyo, huwezi kumpata Mako mpaka yeye akupigie. Ili kuwatoa hofu wazazi, Mako aliwapigia mara moja kila mwezi, akawaambia anaendelea vizuri na mambo yananyooka wasihofu!

Katika jiji kuu la Nchi Yetu, katika uwanja wa Uhuru watu wengi walifurika wakiwemo viongozi wa mataifa mbalimbali. Wote walifika kushuhudia tukio la kuapishwa kwa rais mpya wa Nchi Yetu, Mzee Mnyonge!

Baba alikuwa miongoni mwa watu waliokataa kupitwa na shughuli hii ya kihistoria. Alikaa uwanjani siti ya mbele akilitazama jukwaa alilopaswa kukaa Rais mpya, Mzee Mnyonge. Hata hivyo leo alionekana kuwa makini na asiyeamini alichokiona mbele yake. Alikaa katika mshangao ule kwa saa kadhaa mpaka Mzee Mnyonge alipoapishwa.

Sasa Mzee Mnyonge baada ya kuwa rais mpya, akakaa katika kigoda. Alivaa suruali ya mtumba nyeusi, shati jeupe lililovaliwa mara kadhaa na tai nyekundu ambayo inaonekana alilazimishwa kuivaa ili kuzingatia itifaki. Mkono wa kulia alishika mkuki, kushoto alik**ata ngao iliyochorwa rangi za bendera ya Nchi Yetu. Baba aliendelea kumtazama mtu aliyemtazama kwa muda mrefu. Mtu huyo alisimama nyuma ya rais Mzee Mnyonge. Alivalia kofia ya askari, Koti jekundu lililotiwa nakshi za kijeshi k**a kamba na mikufu iliyotambaa maeneo ya juu. Kijana huyu alikuwa mpambe wa rais, kwa jina la kimombo akiitwa ‘aide-de-camp’ lakini huko mtaani, watu humuita ‘bodigadi’ japo hiyo si kazi yake. Baba alimshangaa sana kijana huyo. Si kwamba alishangaa kijana wa umri mdogo kupewa jukumu hilo kubwa, au alishangaa mavazi aliyovalia la! Baba alimfahamu kijana huyo, alikuwa Mako!

Kuwa wa kwanza kupokea mwendelezo wa riwaya hii kwa kujiunga katika group hili... https://chat.whatsapp.com/EJMKHncJobzH2IhhPVSvCC

22/09/2022

Mzalendo Kizimbani
Sehemu ya Tisa

Katikati ya huzuni baba alipata chembe ndogo ya furaha. Mama aliaga kwamba, kesho angesafiri kwenda kwao kumuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa mahututi. Kusikia hivyo, Baba akasisitiza, “Kesho mapema sana uanze safari. Mama ni Mungu wa pili.” Jambo hili lingempunguzia makelele na maswali arudipo nyumbani. Hata hivyo halikuwa suluhisho la muda mrefu.

Asubuhi Baba alitoka akimsindikiza Mama mpaka kituo cha magari ambako Mama alipanda na kuianza safari. Baba aliendelea na msako wa mtoto wake. Leo alipita kituo hiki cha polisi akaenda kile. Kisha hapa halafu pale, huku tena kule lakini kote alikopita hakumpata mtoto. Tena vituo vingi vilimwambia havijapokea mtoto mahabusu tangu mwaka uanze.

Baba akaanza kutembelea mahospitali, nako hakumpata mwanae. Hakukuwa na dalili, hakukuwa na chochote. Aliyechoka sana, akarejea tena Manunio, barabara ile aliyotupwa na walinzi wa Nchi Yetu, alipofika, hapakuwa na dalili, Mako hakuwako!

Baba alirudi nyumbani kachoka hoi bin taabani, sisimizi mdogo angetosha kumpiga kikumbo na kumdondosha chini, ni bahati tu, sisimizi hawakulijua hilo. Alipitiliza moja kwa moja mpaka chumbani akalala usingizi wa mang’amung’amu, japo hakushusha chandarua, mbu hawakujisumbua kumnyonya damu, walikuwa waungwana, hawakutaka kuongeza matatizo kwa mtu mwenye matatizo.

Saa kumi na mbili asubuhi Baba aliamka. Akaenda moja kwa moja bafuni ambako alifanya shughuli za kusafisha mwili kisha akerejea chumbani akiongea peke yake, “Inawezekanaje mtoto apotee mikononi mwa wanausalama? Wamemuua? Ama wanataka kumfanya muuaji? Wanataka kunitenga naye? Wanataka nini kwa mwanangu? Ndiyo kusema sitamwona tena Mako?”

Baba akavaa nguo zake, shati pana na suruali pana kidogo. Juu akavaa kofia iliyokaa k**a sufuria katika kichwa chake cha duara, halafu akavaa kiatu ambacho huvaliwa na wachezaji wa mpira wa kikapu. Kisha akasikika akisema, “Vita imeanza… dhuluma humfanya mwanadamu awe mwovu.”

Baba akaenda katika chumba anacholala mwanae. Alipofika humo akapatwa na uchungu mkali, akadondoka chini akifikia magoti, akainamisha kichwa chake na kuangua kilio kikubwa!
Akanyamaza ghafla k**a jenereta lililoishiwa mafuta, akaiendea kabati kubwa ambayo huwekwa vitu vya kuchezea mwanae, hapo akaichukua bastola ndogo nyeusi, akaifungua taratibu na kuiweka kipande cha mbao humo ndani ili kuipa uzito unaofaa.halafu akasogea katika kioo, akajitazama kuanzia juu mpaka chini, mkononi akiwa na bastola, akafuta machozi yaliyokuwa yanachuruzika, akacheka! Mara akanuna! Akacheka tena! Akanuna, kisha akawa katika hali ya kawaida.

Baba anayo gari ndogo yenye muundo wa ‘hatchback’, huiendesha kwa nadra sana kwani mara nyingi hupendelea kutumia usafiri wa umma. Yeye husema kuwa, usafiri wa umma ni nafuu kuliko gari binafsi. Aliifuta vumbi, akafungua na kukagua injini, akakagua tairi na kuona mambo yako sawa, akakaa nyuma ya usukani, akaiwasha, akaiacha ichemke kidogo, akakanyaga breki, halafu gia akaisogeza palipoandika D, akaachia breki, gari ikaserereka, akakanyaga pedali nyingine, gari ikaserereka zaidi.

Baada ya kuendesha kwa muda, alikunja kushoto akaiingia barabara iliyoelekea Poste. Akaendelea kuendesha mpaka alipofika katika kituo cha daladala, akashuka na kuiacha gari mahali pale.

Alitembea taratibu akiangalia askari waliolinda benki ile. Walikuwa wawili, mmoja ana bunduki, akaona si rahisi kuwavamia, akatembea taratibu akifuata njia iliyonyooka, halafu akakunja kushoto, akatembea hatua k**a sitini na tano hivi na kuufikia ubalozi wa Ufaransa. Hapo napo akaona askari wawili, mmoja ana bunduki, mwingine hana. Alipokutanisha nao macho, akavuka barabara, akazunguka na kurudi pale alipoegesha gari. Kisha akaona jambo la kuvutia, askari mmoja hakuwepo, yule mwenye bunduki aliiegesha katika bega, na alikuwa amesogea usawa wa barabara tena anaongea na simu akiwa kachuchumaa. Alisogea taratibu mpaka usawa wa askari yule, akasimama mbele yake, askari alipoinua uso, akakutana na mdomo wa bastola. “Tulia hivyo hivyo… ukijitingisha namwaga ubongo wako,” ilisikika sauti, kisha bunduki ile aina ya SMG ikapigwa teke na Baba na kudondoka chini, baada ya Baba kuona askari yule akitetemeka, aligundua asingeweza kumletea shida, hivyo akaiokota SMG na kuivaa kamba ikishika bega la kushoto na kuzuiwa na shingo, silaha ikining’inia upande wa kulia. Baba hakuchelewa, akatoa pingu na kumfunga askari yule aliyekuwa akitetema k**a trekta. Haraka aliyefungwa pingu, askari akaingizwa nyuma ya mlango wa ngari ndogo ya Baba, alipomfikisha hapo, akamsukuma na kuufunga halafu akaingia na kumfunga kamba za miguu pamoja na plasta ngumu mdomoni, halafu akamuonya, “Sisi ni genge baya, ukijaribu kuleta ujanja, tutafyeka ukoo wako mzima, sawa poti?” Poti akakubali kwa kutikisa kichwa, Baba akaiwasha gari na kuendesha.

Inaendelea...

Kuwa wa kwanza kupokea mwendelezo wa riwaya hii kwa kujiunga katika group hili... https://chat.whatsapp.com/EJMKHncJobzH2IhhPVSvCC

14/09/2022

Mzalendo Kizimbani

Sehemu ya Nane

Mara baada ya kukitoka chumba cha mahojiano, Baba alivikwa kitambaa cheusi. Akaongozwa na watu wawili mpaka ndani ya gari muundo wa SUV nyeusi. Waliendesha mpaka mahali ambapo Baba alivuliwa kitambaa hicho, breki zikakanyagwa, mlango ukafunguliwa halafu akasukumwa nje akadondoka k**a mzigo. Isingekuwa tabia ya kufanya mazoezi na kula mlo sahihi, Baba angevunjika mfupa wa paja.

Baba akiwa chini, alishuhudia gari ikienda mbele, kisha ikakunja kona na kurudi ilipotoka, ikampita kwa kasi ikimtimulia vumbi. Alifanikiwa kumuona dereva wa gari ile, kijana mdogo mwembamba, nywele zake fupi, bila shaka hata aliyemsukuma naye alikuwa kijana mdogo tu.
Hata akawaza hasa k**a vijana wale walitambua maana ya kuaminiwa na kuwa sehemu ya usalama wa Nchi Yetu. Halafu akawaza, vipi k**a mwanaye angeshushwa kwa mtindo ule, mifupa yake laini, mtoto Mako asingeweza kuhimili!

Baba alijizoazoa pale chini aliyekatishwa tamaa na walioaminiwa kutulinda. Aliposimama akapiga mikono yake akitingisha kichwa ishara ya kukata tamaa. Akaanza kutembea akijaribu kutafakari ni wapi mahali hapo. Alitembea mwendo mfupi akiifuata barabara ile ya vumbi, mbele akaiona barabara ya lami na k**a bahati akaiona daladala iliyosimama ikisubiri wapandaji. Konda alimuona Baba. “Dingii, Kumbukumbu unaenda?”

Kusikia hivyo, Baba akaongeza mwendo na kuingia ndani ya daladala ile. Alibaini kuwa, mahali pale palikuwa Manunio. Akiisha kukaa katika kiti, mwisho kabisa wa daladala tena dirishani, akatazama njia ya vumbi alikotokea, kule alikosukumwa na vijana wadogo walinzi wa usalama wa Nchi Yetu, kwa sauti ya chini, akakohoa laana, akawalaani vijana wale, akawaombea jambo baya liwakute. Kisha akaganda k**a barafu gari ilipoanza kuelekea Kumbukumbu.

Alipofika kumbukumbu alipanda gari nyingine iliyompeleka nyumbani kwake. Alifika nyumbani saa moja usiku, akaingia chumbani akimpita Mama aliyekaa sebuleni. Mama alisubiri dakika mbili, kisha akapaza sauti, “Mmeondoka wawili umerudi peke yako. Mtoto yuko wapi?”

“Dume lile. Limechukuliwa na baba yake mdogo, litakuwa limeshafika Magomeni muda huu,” Baba alidanganya. Mama akanyamaza, maamuma asiyejua kitu.

Kulikucha asubuhi, Baba akakaa nje akisubiri kumuona mtoto akiletwa au akija peke yake. Asubuhi ikapita bila mtoto kufika. Ukafika mchana, mtoto hakufika, kuelekea jioni, Baba akakodi gari binafsi mpaka Manunio, kule alikotupwa na wale vijana wadogo. Alifika eneo lile, akakagua, lakini hapakuwa na dalili ya kushushwa mtu. Hapakuwa na dalili ya nyayo za Mako.
Baba akarejea nyumbani.

Baba alimpita Mama sebuleni, akaenda moja kwa moja mpaka chumbani. Mama akapaza sauti, “Baba mdogo alifika hapa kututembelea jioni. Ulipotoka yeye akaingia. Nimemuuliza mbona kaja peke yake bila mtoto hajajibu. Sasa nieleze, mtoto yuko wapi?”

“Kwani mwanao ana baba wadogo wangapi?” Baba aliuliza.

“Wengi.”

“Sasa huyo Baba mdogo aliyekuja una uhakika gani kuwa ndiye aliyemchukua mtoto?”
“Ulisema Magomeni, wa Magomeni kaja.”

“Nilisema atakuwa ameshafika Magomeni, yaani katikati ya safari yake kulekea Magambani.”
“Ahaaa kumbe kaenda kwa baba yake wa Magambani Mwasonga! Basi nikawaza sana…”

“Acha hizo, toto la kiume halichungwi,” Baba alihitimisha. Lakini atadanyanya mpaka lini? Njia ya muongo fupi!

Inaendelea...

Inaendelea...
Kuwa wa kwanza kupokea mwendelezo wa riwaya hii kwa kujiunga katika group hili... https://chat.whatsapp.com/EJMKHncJobzH2IhhPVSvCC

06/09/2022

Mzalendo Kizimbani
Sehemu ya Saba

Baba na mwana walitolewa uwanjani katika namna ambayo watu wengi hawakuelewa. Zoezi liliendeshwa taratibu, wachache walishangazwa lakini wakapuuza kwani hakukuonekana purukushani yoyote. Vyombo vya usalama vya nchi yetu huwa havipuuzi kitu. Japo jambo hilo lilionekana dogo, huku nyuma ulinzi uliimarishwa mara dufu!

Baada ya kutembea kwa gari kuelekea kusikojulikana, hatimaye Baba na mwana waliingizwa ndani ya chumba kilichokuwa na viti vinne na meza moja. Walikwenda moja kwa moja wakakaa katika viti viwili vilivyofuatana.

“Dogo,” baba aliita, akamtazama mwanae aliyekaa tulivu katika kiti. “Hiki ni chumba cha mahojiano, jamaa wametuhisi vibaya kuhusu ile darubini yetu na tuliyokuwa tukizungumza uwanjani.”

“Watatufanya nini?”

“Watatuhoji. Sema ukweli tu, usidanganye jambo hata moja… nami nitasema ukweli. Lakini nitawasumbua kidogo.”

“Ha ha haaa!” Mtoto alicheka, halafu akauliza, “Tutakaa humu mpaka saa ngapi?”

“Muda wowote watakuja kutuhoji. Lazima wawe wawili. Mmoja anasimama k**a shahidi wa mwingine. Halafu wamekosea, hatukutakiwa kuwekwa sehemu moja, ilitakiwa wewe ukae peke yako na mimi peke yangu.”

Baada ya saa mbili za kuwa ndani ya chumba, waliingia watu wawili k**a alivyosema Baba.
Wote walivalia suti nyeusi na walikaa katika viti viwili vilivyosalia hata wakawa wanatazamana uso kwa uso na washukiwa wao. Katika watu hawa wawili walioingia, mmoja alikuwa mnene na mwingine mwembamba. Yule bwana mnene akachomoa bastola na kuiweka mezani. Baba kwa masikitiko, akaweka kiganja cha mkono wake juu ya macho ya mwanaye, hakutaka aone jambo hilo. Bwana mnene kwa kutambua hilo, akaitoa silaha na kuirejesha kiunoni, Baba naye akatoa viganja juu ya macho ya mtoto.

Yule bwana mwembamba akamkazia macho baba na kumuuliza, “Naweza kukuuliza maswali?”
“Unaweza kuniuliza maswali mengi utakavyo. Lakini siwezi kujibu mpaka awepo mwanasheria wangu,” baba alijibu kwa kujiamini, mtoto akatabasamu.

“Unaweza kuwasiliana na mwanasheria wako ili tukuhoji ukiwa naye?” bwana mnene aliongeza.
“Hapana… sina mwanasheria,” baba alijibu, safari hii mtoto hakuishia kutabasamu, akaangua kicheko.

“Unajua kwa nini uko hapa?” mwembamba aliuliza.

“Hapana.”

“Umetumwa na nani kumdhuru mtawala wetu?”

“Sijatumwa na mtu, wala sina nia ya kumdhuru mtawala.”

“Maarifa gani yalikupa ufahamu wa mapungufu ya walinzi wa watawala?”

“Swali limezunguka sana. Lakini mimi husoma katika vitabu kujipatia maarifa pekee. Yote ninayoyafahamu hayahusiani na kundi lolote ovu.”

“Kwa nini unachunguza masuala ya usalama wa mtawala?”

“Ni kiongozi wangu, sioni ubaya nami kuhakikisha kweli yupo salama.”

“Jina lako nani?”

“Baba,” Baba alijibu.

“Baba nani?”

“Baba Mako.”

“Jina la tatu?”

“Baba. Sasa kamilisha hivi: Baba Mako Baba.”

“Mtoto jina lako nani?” Mnene aliuliza akitabasamu.

“Siwezi kujibu chochote bila mwanasheria wangu,” mtoto alijibu.

“Mpigie simu mwanasheria wako aje.”

“Sina mwanasheria,” mtoto alijibu. Baba akamtazama, akaangua kicheko.

“Jina lako nani?”

“Mako.”

“Jina la pili.”

“Ongeza jina la huyu mzee.”

“Jina la tatu?”

“Shuleni jina langu kamili ni hilo, sina jingine.”

“Ulijifunza wapi kuhusu usalama wa watawala na mapungufu yake.”

“Kanifundisha Baba.”

“Yeye kajifunza wapi?”

“Kuna wakati husoma vitabu, kuna wakati hutazama mtandaoni na kuna wakati hutunga hoja zake mwenyewe.”

“Una miaka mingapi?”

“Saba.”

“Unasoma darasa la ngapi?”

“Darasa la pili.”

“Asante kwa ushirikiano,” Mwembamba alisema akimshika mkono Mako.

“Baba upo huru kurejea nyumbani,” Mnene alizungumza, Baba akamshika mkono mwanaye ili watoke. “Mtoto bado tuna mahojiano naye, atarudi yakikamilika,” Mwembamba alisisitiza akiamuru Baba aondoke mwenyewe.

Baada ya mabishano ya muda, Baba alikubali kuondoka. Siyo kwa sababu alizidiwa hoja, lakini hakuwa na nguvu za kuweza kutoka na mwanaye. Kwa upole akaaga, “Baki salama Mako… Sema ukweli, usiwasumbue bila mimi kuwepo watakuumiza ukileta mchezo,” mtoto asiyeamini k**a alitakiwa kusalia mule akajibu kwa upole, “Sawa.”

Inaendelea...

Kuwa wa kwanza kupokea mwendelezo wa riwaya hii kwa kujiunga katika group hili... https://chat.whatsapp.com/EJMKHncJobzH2IhhPVSvCC

01/09/2022

Mzalendo Kizimbani
Sehemu ya Sita

Baba na mwana walikaa katika viti vya rangi ya machungwa katika jukwaa la uwanja wa mpira. Hawakuwa peke yao, watu wengine walifurika katika uwanja huo. Baba na Mwana walikuwa juu kwa idadi ya ngazi tano kutoka mwanzo na mbele yao walilitazama jukwaa la VIP, katika jukwaa hili wangekaa watu waliozaniwa kuwa muhimu ilihali afya zao ziliashiria bado kidogo wa RIP.

Baba alivaa fulana nyeusi, kaptura ndefu ya michezo na chini alivalia makubadhi ya kisasa. Mtoto alivalia suruali ya kubana aina ya ‘traki’, juu alivalia sweta lililoendana na traki yake na rangi yake kijivu, chini alivalia k**a baba yake, makubadhi ya kisasa. Wote baba na mwana, sura zao nzuri za kupendeza na juu walifunika vipilipili vyao kwa kuvalia kofia. Baba akivalia kofia nyeusi, na mtoto akivalia kofia nyekundu lakini yenye mistari ya bluu na kutengeneza kitu mfano wa drafti.

Ilikuwa siku ya kusherekea uhuru wa Nchi Yetu, watu wengi walikusanyika ili waweze kushuhudia maonyesho hayo. Ilitakiwa kuingia mapema uwanjani, lasivyo ungeikosa nafasi.

Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Nchi Yetu, mfupi mnene, jina lake Makapa. Baba na Mwana walifika uwanjani saa mbili asubuhi, na sasa ilitimia saa tano asubuhi na mgeni rasmi alikuwa bado hajafika. Hata hivyo, dalili zilionyesha kuwa, muda wowote Rais Makapa angefika.

Hayawi hayawi hatimaye yalikuwa; aliyesubiriwa sasa alifika. Rais Makapa aliingia akisindikizwa na walinzi wengi, watu wengi uwanjani walisimama kumshangilia, mtoto alipotaka kusimama, baba yake alimshika mabega na kumtaka aendelee kukaa. Halafu akasema na mwanaye, “Wengi wanaosimama wamelipwa, usifuate mkumbo!”

Baada ya shamrashamra za kumkaribisha rais, watu walikaa na ratiba ya maonyesho ikasomwa. Watu walisubiri kwa hamu maonyesho ya Makomandoo yakivunja tofali kwa vichwa na kukaa juu ya misumali. Hata hivyo, tangu wakiwa nyumbani Baba alimweleza mwanae kuwa, tofali wanazovunja Makomandoo hao ni mbichi, hata yeye akipewa anavunja, mtoto hakuelewa, akacheka.

Jukwaa walilokaa baba na mtoto lilitazamana na jukwaa alilokaa rais Makapa.
“Dogo…” baba alimuita mwanae.

“Naam…” mtoto aliitika. Baba akaendelea, “Unaona pale alipokaa Rais Makapa?”
“Ndiyo.”

“Pale analindwa kwelikweli. Ulinzi wake upo katika duara mbili…” baba alieleza, kisha akatoa karatasi na kalamu akaanza kumchorea mtoto huku akizungumza, “Duara la kwanza ni wale jamaa unaowaona karibu yake, unawaona vizuri… wale wenye suti nyeusi, wembamba.”

“Nawaona, lakini natamani ningesogea karibu zaidi ili niwaone vizuri,” alijibu mtoto, baba akatoa darubini kwenye mkoba akampatia. “Chukua hii, sasa tazama unaona vizuri.”

“Ndiyo…” mtoto alijibu akitazama katika darubini. Halafu akaishusha ili kumsikiliza baba.

“Sasa, lile ndiyo duara la kwanza. Duara la pili wapo mbali kidogo. Unamuona yule kulee, duara la pili yule… tazama kwenye darubini, yule kule kwenye kona ya mlango… hebu nipe na mimi nimtazame vizuri… asante… haya na wewe tazama.”

“Unawezaje kuwatambua?” aliuliza mtoto.
“Nywele zao fupi, wamevaa suti na namna wanavyosimama. Lakini wengine hatuwezi kuwatambua. Wamevaa k**a sisi na wamejichanganya humuhumu.”

Baba alikohoa, akafikicha macho kidogo halafu akazungumza, “Kuna kosa la usalama naliona, pakitokea mtu mwenye nia mbaya anaweza kummaliza kiongozi wetu.”

“Kosa gani?” aliuliza mtoto.

“Kosa lililofanywa na walinzi wa Muhammad Anwar el-Sadat. Unakumbuka nilikusimulia namna rais huyu alivyouawa akiwa uwanjani kwenye tukio k**a hili la leo.”

“Ndiyo nakumbuka!”
“Sasa nyanyua darubini yako, tazama halafu uniambie makosa unayoyaona,” alisisitiza baba, mtoto akanyanyua darubini akatazama kwa udadisi. Baada ya muda akasema, “kwanza kiongozi katika eneo la mbele hana kitu kinachomzuia asipigwe risasi, hata mimi naweza kushambulia ukizingatia getini tulipita bila ukaguzi wowote. Pili naona magari ya majeshi hayana alama yoyote zaidi ya rangi ya kijani. Wahalifu wanaweza wakaingia na magari yanayofanana na yale ya kijeshi, watu wote na vyombo vya usalama vikajua ni sehemu ya maonyesho, halafu wahalifu hawa wanaweza kusogea karibu kabisa na kiongozi wetu kwa mwendo wa haraka na kumsababishia madhara. Kingine naona kosa kubwa sana, hili…” hakumaliza kauli yake, mtoto alinyang’anywa darubini na mwanamume mrefu aliyevalia suti, alipotazama mbele, alimuona baba yake akikokotwa na jamaa mwingine mrefu, walipokutanisha macho baba akatabasamu hata hivyo tabasamu lake liliashiria alikuwa katika matatizo.

Inaendelea...

Kuwa wa kwanza kupokea mwendelezo wa riwaya hii kwa kujiunga katika group hili... https://chat.whatsapp.com/EJMKHncJobzH2IhhPVSvCC

23/08/2022

Mzalendo Kizimbani
Sehemu ya Tano

Akiendelea kujivuta, alifika sehemu ambayo kamba ilikuwa karibu zaidi na maji. Mamba mmoja akaruka kiasi cha kumkaribia, akachomoa bisu lake na kuliachia liingie ndani ya mdomo wa mamba yule, mamba kwa kukwamwa na lile bisu akayapiga maji kwa nguvu, Ado akajitahidi kujivuta, lakini kwa sababu ya mtikisiko ule, kamba ilianza kuachia taratibu upande wa ng’ambo alikoelekea.

Wenzake walishazishika bunduki zao na walielekeza alikokuwa, hata hivyo hakuna ambalo wangeweza kufanya, haingekuwa rahisi kulenga shabaha kumpiga mamba, kosa dogo lingesababisha risasi impate Ado.

Ado alipogundua kamba inaachia, akaanza kujivuta kwa kasi zaidi. Akajivuta… akajivuta… mpaka akautoka mto, akaendelea kujivuta mpaka alipolifikia tawi la mti ambalo ncha ya kamba ilijishikiza. Haraka akak**ata tawi, halafu akaichomoa kamba ile na kuifunga upya, safari hii kwa uimara zaidi. kisha akawafanyia ishara wenzake, ishara ya kupiga mluzi ulioashiria njooni wote kamba ipo imara.

Alianza Mako, akafuatiwa na Bwii, nyuma ak**alizia Moli. Kamba ilikazwa ikawa juu zaidi hivyo hapakuwa na hofu tena ya kuguswa na wale mamba. Makomandoo walijivuta kwa kasi na tazama, kufumba na kufumbua walikuwa ng’ambo ya mto. Juu ya tawi imara la mti. Walishuka bila kuitoa kamba ile, pengine waliamini wangeitumia baadae wakati wa kurudi.

Sasa makomandoo walikuwa chini ya mti, walipanga namna ya kushambulia kwani tayari eneo la tukio walishalitambua.

Ado na Moli walichukua nafasi. Wote walilala chini na Ado alikuwa ameishika vyema bunduki yake, Barrett M82. Bunduki hii imekuwa kipenzi cha wadunguaji wengi. Silaha hii ina historia ya kustaajabisha. Ilitengenezwa na Bwana mmoja aitwaye Ronnie Barret ambaye alifanya kazi ya kupiga picha na hakuwahi kuwa na uzoefu wa masuala ya silaha. Pamoja na kukosa ujuzi huo, aliweza kutengeneza silaha hiyo akiwa katika gereji yake tena kwa kutumia vifaa vya humohumo gereji. Baadae silaha hii ilijipatia umaarufu na kuanza kuboreshwa zaidi na serikali ikiwemo Marekani.

Makomandoo waligundua kwamba, maadui walikuwa wawili pekee ambao hata hivyo walikuwa mahali pale kwa muda tu na pengine kuna sehemu walitamani kuwafikisha mateka wao.

Watekaji walikuwa wakizunguka hapa na pale na waliweza kuonekana kupitia dirisha dogo. Ado na Moli walisubiri angalau mtekaji mmoja asimame katika usawa wa dirisha kwa angalau sekunde tatu ili waweze kumpiga risasi. Walisubiri kwa muda mrefu na sasa Ado alichoka akamwachia Moli ambaye alilala nyuma ya Barret M82, jicho moja likitazama katika darubini ndogo ya silaha hiyo.

Haikuchukua muda tangu silaha iwe mkononi mwa Moli jambo lililotarajiwa kutokea. Adui alisimama usawa wa dirisha, hakutoka usawa huo, aliganda kwa sekunde zilizotakiwa, halafu ukasikika mlio, “Tuuuuuh…” mtekaji mmoja akadondoka, lakini kumbe chini ya dirisha alikuwepo Bwii, kwa kuwa adui mmoja alibabaishwa na kuanguka kwa mwenzake, Bwii akapanda juu ya dirisha akiwa kaishika bastola aina ya Sig Sauer, akapiga risasi, adui wa pili akadondoka. Wazalendo wakaokolewa!

Ilikuwa furaha katika kambi ya muda baada ya kuwaona Makomandoo wakirudi na askari wawili waliotekwa na waasi. Wazalendo walipongezwa kwa ushujaa wao, waliookolewa wakakumbushwa kuwa, hawakuwa mateka tena na wawe tayari kuendelea na majukumu yao.
Siku iliyofuata, Komandoo Mako, Bwii, Ado na Moli wakarejea nyumbani, wakarejea katika Nchi Yetu, wakiwa kifua mbele kwa uzalendo uliotukuka. Sasa wamo katika dege la kijeshi na muda si mrefu watatua nyumbani.

“Wazee…” Mako alivunja ukimya, wenzake wakamsikiliza kwa makini kwa sababu alionekana anataka kuongea kitu cha maana. Alipoona wote wako makini kumsikiliza, akatengeneza sauti yake, halafu akawatazama kwa sekunde tatu, kisha akasema, “Nilikuwa siamini k**a kila kitu kinawezekana hapa Duniani mpaka siku nilipoota nakimbizwa na konokono.”

Makomandoo wakacheka, walizani jambo la msingi kumbe ulikuwa mzaha tu.

“Nisikilizeni,” alidakia Ado, akiwa bado anacheka, halafu akaendelea. “Leo nimegundua maana ya ujinga. Ujinga ni kumaliza darasa la saba bila kujua sifuri inaandikwaje katika namba za kirumi.” Makomandoo wakatazamana, halafu wakacheka.

“Hivi sifuri inaandikwaje kwa kirumi,” aliuliza Moli.

“Humu wote wajinga, hata rubani pale mbele hajui.” Alidakia Bwii, wote wakacheka, hata rubani wa dege lile la kijeshi, mzalendo Tata Marwa, akacheka. halafu dege likaanza kutua, wazalendo wamerudi nyumbani.

Inaendelea...

Kuwa wa kwanza kupokea mwendelezo wa riwaya hii kwa kujiunga katika group hili... https://chat.whatsapp.com/EJMKHncJobzH2IhhPVSvCC

19/08/2022

Ni vigumu kutabiri, hasa k**a utabiri huo unahusu mambo yajayo.

18/08/2022

Hatujapotea. Tuna changamoto ya kujua mahali tulipo.

17/08/2022

We live, we love, we lie.

16/08/2022

You should be friendly, but not become friends, with students.

Want your school to be the top-listed School/college in Dar es Salaam?

Click here to claim your Sponsored Listing.

Location

Category

Telephone

Address


Kinondoni Manyanya
Dar Es Salaam
0701072