Maskani ya Vitabu na Maarifa

Maskani ya Vitabu na Maarifa

Share

🎯 Vitabu
🎯 Maarifa
🎯 Maendeleo binafsi

28/04/2026

TABIA ZA FURAHA

Dean Graziosi katika kitabu chake *Millionaire Success Habits*, anaeleza kuwa moja ya tabia za watu wanaofanikiwa ni kutumia nguvu ya furaha.

Watu wanaofanikiwa hawasubiri mafanikio ili wapate furaha. Wanatumia furaha k**a msukumo wa kufikia mafanikio.

Na kosa kubwa ambalo watu wengi hufanya…

…huishi wakiamini; wakifanikiwa, ndipo watakapokuwa na furaha.

Lakini ukweli hata wanapopata kile walichokuwa wanakitafuta, furaha wanayoipata huwa ya muda mfupi. Baada ya muda wanazoea walichokifika, kinaonekana cha kawaida na furaha hupotea.
_________

Furaha ya Nje Dhidi ya Furaha ya Ndani.

Ulimwengu wa nje unajumuisha vitu k**a; mali, kipato kikubwa, afya, fedha, elimu, kazi, uhusiano, ambavyo vinaweza kuleta furaha, lakini mara nyingi huwa ya muda mfupi.

K**a mtu hana mtazamo wa furaha kutoka ndani, hata akiwa na kila kitu bado atahisi upungufu.

Lakini mtu anapojifunza kuwa na furaha kutoka ndani bila kutegemea hali, bila kutegemea vitu, bila kutegemea matokeo, furaha hiyo hugeuka kuwa chanzo cha kupata hata hivyo vitu vya nje.
________

Tabia 10 za Furaha

Tabia ni matokeo ya kufanya jambo mara kwa mara mpaka linakuwa sehemu ya maisha yako, unalifanya bila kutumia nguvu kubwa ya akili na hata kutojisikia sawa usipolifanya.

Kwa hiyo, kuna tabia ambazo hufanya furaha iwe sehemu ya maisha ya mtu na si tukio la muda.

1. Kutafsiri furaha yako

Jiulize, furaha kwako ina maana gani? Ni hali gani imewahi kukupa amani ya kweli? Ni kitu gani kiliwahi kuwasha moyo wako?

Kisha andika orodha ya mawazo, mambo unayoshukuru, shughuli zinazokupa hali hizo hapo juu. Ukifanya hivyo unajenga msingi wako wa furaha.

2. Ishi kwenye wakati wa sasa

Eckhart Tolle katika kitabu chake *The Power of Now* anaeleza kuwa kuishi kwenye sasa huleta amani ya ndani. Usiishi kwenye jana (majuto), wala kwenye kesho (hofu), ishi kwenye leo yako, hapo ndipo furaha ipo.

3. Usifikirie kupita kiasi

Tafuta maarifa yanayokupa ujasiri, jisikilize kutoka ndani, kisha chukua hatua kwani kufikiria sana bila kuchukua hatua kunaua furaha.

4. Weka shabaha kwenye matokeo chanya

Achilia mawazo hasi, kubali kuwa si kila kitu kiko ndani ya udhibiti wako, na waza yaliyo chanya yanayowezekana.

5. Usijipe matarajio makubwa sana

Tony Robbins aliwahi kusema:
> “Maisha ni kwa ajili yetu, na si yetu.”
Wakati mwingine mambo hayaendi k**a ulivyopanga lakini baadaye ndipo unaona uzuri kwenda kwake kinyume.

6. Shinda hofu ya kushindwa

Acha kuamini kuwa kushindwa ni kitu kibaya. Winston Churchill alisema;
> “mafanikio ni kuendelea kutoka kushindwa hadi kushindwa bila kupoteza hamasa”,
Na Thomas Edison alisema;
> “hakushindwa, bali aligundua njia elfu kumi zisizofanya kazi”
Hivyo mtu asiyeshindwa hajaribu vitu vipya, anaishi kwenye eneo la faraja, chukulia kushindwa k**a sehemu ya safari.

7. Jifunze kupotezea

Usiwe mtu wa vinyongo kwani kinyongo hakimdhuru mwingine, kinakuumiza; samehe, achilia na linda furaha yako.

8. Shukuru kwa kile ulichonacho

Shukuru hata kwa mambo madogo k**a pumzi, chakula, maisha, kwani shukrani huongeza furaha.

9. Usibweteke

Endelea kusonga mbele kwani kisaikolojia furaha huongezeka kadri mtu anavyokua na kupiga hatua, na kudumaa kunapunguza furaha.

10. Imani
Imani kwa Mungu huleta utulivu, amani ya ndani, usalama wa moyo, na huwa nanga wakati wa misukosuko ya maisha.
_________

Mwisho

Furaha si kitu kinachosubiriwa kuja baada ya mafanikio, bali ni mtazamo unaojengwa na tabia inayolelewa.

Ukiweza kuijenga ndani yako, kuilinda, na kuishi nayo kila siku, basi mafanikio hayatakuwa tena chanzo cha furaha yako, bali yatakuwa matokeo ya furaha uliyonayo tayari.

27/04/2026

VIPI K**A?

Linaonekana ni swali dogo, lakini lina uzito mkubwa kuliko linavyoonekana: “Vipi k**a?”

Ni swali ambalo karibia kila mtu katika nyakati fulani za maisha yake hujiuliza…

…nyakati za maamuzi magumu, nyakati za kuendea asichokuwa na uhakika nacho, nyakati za kutafakari maisha yake, nyakati za uchukuaji hatua, fursa.

Ni swali linaloweza kuamua mwelekeo mzima wa maisha, kuwa kizuizi au mlango.

Swali hili mtu hujiuliza kabla, wakati na hata baada ya jambo kutendeka.

Swali “Vipi k**a?” ni chanzo cha nguvu, ujasiri, uthubutu mtu anapojiuliza na kusudio la uwezekano…

…ni kizuizi mtu anapojiuliza akiwa na mtazamo hasi.

Pia ni majuto, mtu anapojiuliza wakati ambao hakufanya ilivyopasa.
________

Haya ni baadhi ya maswali yake;

Hofu:
•Vipi k**a nitashindwa?
•Vipi k**a nitakosea?
•Vipi k**a hakuna atakayeniunga mkono?
Vipi k**a nitaanza halafu nikaanguka?
•Vipi k**a nitakataliwa?
•Vipi k**a nitapoteza na hiki?

Mtazamo Chanya:
•Vipi k**a nitafanikiwa?
•Vipi k**a hii ndio nafasi pekee?
•Vipi k**a nikijaribu tena?
•Vipi k**a nikianza leo?
•Vipi k**a nisipokata tamaa?
•Vipi k**a nitasamehe tu
________

…watu walioweka rekodi za muda wote, mafanikio makubwa waliyofikia, ni kwa sababu waliangalia upande chanya wa swali hili.

Maisha, uwezo, na vipaji vyao walivitumia kitimilifu na swali “Vipi k**a?” si la majuto upande wao.

Ushawahi Kujiuliza?

•Vipi k**a mama angesema “siwezi tena” alipokuwa akiambiwa sukuma?

•Vipi k**a Julius Nyerere asingesimama kuongoza kudai uhuru?

•Vipi k**a John Magufuli asingechukua maamuzi magumu aliyochukua?

•Vipi k**a Mohammed Dewji angehofia kupanua biashara zake nje ya mipaka?

•Vipi k**a Nelson Mandela angekata tamaa akiwa gerezani?

•Vipi k**a Elon Musk angeacha baada ya kushindwa mara kadhaa?

•Vipi k**a Oprah Winfrey angeamini maneno ya waliomdharau?

•Vipi k**a watu hawa wote na wengine wangechagua upande wa hofu wa swali hili?

•Vipi k**a wangekata tamaa kwa sababu ya changamoto walizokumbana nazo? Historia yao ingekuwaje?

•Vipi k**a wewe ndiye uko kwenye nafasi hiyo sasa?

•Vipi k**a dunia inasubiri uamuzi wako, k**a ilivyowasubiri wao?

______

Swali “Vipi k**a” halina ukomo, linabadilika tu na wakati.

Leo utajiuliza “Vipi k**a nitashindwa?”
Kesho utajiuliza “Vipi k**a ningejaribu tu?” na maumivu ya kushindwa hupita, kwa kuwa kushindwa ni sehemu ya kujifunza…
lakini maumivu ya kutojaribu kabisa yanaweza kubaki nawe hadi siku za uzee wako.

Kila mtu unayemwona amefika mbali, aliwahi kusimama mahali ulipo sasa… akiwa na swali hilohilo, tofauti ni kwamba alishinda hofu, hakuruhusu changamoto ziwe mwisho wake.

23/04/2026

HAJA YA NAFSI:
Ukweli kuhusu Njaa ya Ndani

Kuna aina ya njaa ambayo si ya tumbo wala chakula bali ya nafsi, njaa hiyo ni haja ya kutambuliwa.

Haja ya nafsi ni hitaji la kibinadamu la kawaida kabisa. Kila mtu kwa kiwango fulani huhitaji kutambuliwa, kuthaminiwa, kuonekana, na kukubalika kwa vile alivyo, vile alivyonavyo na vile anavyofanya.

Tatizo halipo kwenye kuwa na hitaji hilo bali pale linapozidi mipaka ya kawaida, na kuwa msingi wa thamani binafsi na kukuendesha...

…husababisha kupoteza uhuru wa ndani, na utambulisho.
_________

Viashiria vya Haja ya Nafsi Iliyokithiri

1. Maamuzi yako yanaongozwa na macho ya watu.
Maamuzi yako msingi wake ni watu, kwamba utatazamwaje na kufikirikaje na wengine na sio uhitaji, kusudi, uhalisia, thamani, mazingira, faida, madhara n.k

2. Unahisi kutoridhika usiposifiwa

3. Unalinganisha maisha yako na ya wengine kila wakati.

4. Unatumia zaidi ya uwezo wako ili kuonekana tu.

5. Huwezi kufanya mambo kimya kimya
Kila hatua lazima uionesha, uhakikishe inajulikana hata k**a hakuna uhitaji wa kufanya hivyo.
_________

Madhara ya Haja ya Nafsi Iliyokithiri.

1. Kupoteza uhuru
Unakuwa mfungwa wa maoni ya watu; furaha, maana na thamani yako, ya kile ulichonacho na unachofanya inatokana na maoni ya wengine si wewe wala ndani yako.

2. Matumizi mabaya ya fedha
Matumizi ya fedha yanakuwa ya kujionesha, ambayo husababisha kuingia kwenye madeni, kushindwa kufikia uhuru wa kifedha na hata utajiri.

3. Kupuuza wajibu stahiki na wa kimsingi.
Kujenga picha nje (kwa watu na maeneo mengine) na kushindwa kuwajibika ndani (kwa familia, ndugu wa karibu)

4. Kupoteza utambulisho halisi
Kadri unavyojionesha, na inapobidi kuigiza ndivyo unavyojitenganisha na wewe halisi.

5. Kukosa amani ya ndani
Unakuwa kwenye hali ya utumwa ambayo huondoa amani.

6. Kujikwamisha.
Kuonesha mambo kabla ya wakati wake, ambayo hutoa nafasi kwa maadui ya kuharibu.
________

Namna ya kudhibiti Haja ya Nafsi Iliyokithiri

1. Jifunze kujithibitisha mwenyewe.
Usisubiri watu wakwambie wewe ni nani. Tengeneza misingi na vigezo vyako binafsi vya kutafsiri utambulisho na thamani yako.

2. Tenganisha thamani na mwonekano.
Hujipatii thamani kwa kujionesha isivyostahili, bali kwa kujenga utambulisho halisi, thamani ya dhahabu haiongezeki kwa kuoneshwa zaidi.

3. Punguza utegemezi wa sifa za nje.
Fanya mambo mazuri hata k**a hakuna anayekuona. Tabia na uhuru wa ndani hujengwa namna hiyo.

4. Wekeza kwenye maarifa, ujuzi, afya, familia badala ya kujionesha.
_________

Hitimisho.
Jioneshe inapopaswa na inavyostahili, jioneshe na onesha kwa kusudi, uthabiti, na uhuru sio kwa shinikizo la macho ya watu.

18/04/2026

SANAA YA KUTOKUJISHIK**ANISHA: Njia ya Wanafalsafa Kulinda Furaha na Uhuru wa Ndani

Kuna ukweli ambao wengi huukwepa, japokuwa uko wazi kabisa:
kila kitu tulicho nacho kina ukomo.

Vitu, watu, nafasi, na vyeo–vyote huja, na kwa namna hiyo hiyo, vinaweza kuondoka.

_____

Mwanafalsafa hulikubali hili mapema. Hujifunza kuishi bila kujifungamanisha navyo, ili vinapoondoka, visiwe na athari ya kuvunja nafsi yake. Ndiyo maana Seneca aliwahi kusema:

> “He who has learned how to be poor has unlearned how to be a slave.” (Aliyejifunza jinsi ilivyo kuwa maskini, ameondokana na jinsi ilivyo kuwa mtumwa.)

Kwa nyakati fulani, Seneca alichagua kuishi maisha ya kawaida kabisa–kulala chini, kutembea kwa miguu, na kula chakula rahisi.
Si kwa sababu alikosa uwezo, bali kwa sababu alitaka kuizoeza akili yake ukosefu.

Alijifunza jambo moja la msingi:
uhuru wa kweli hautegemei kile ulichonacho, bali namna ulivyo.

_____

Kwanini Usijishik**anishe?

Unapojifungamanisha sana na kitu–iwe ni mali, cheo, au mtu; unakipa mamlaka juu ya hisia zako. Unakifanya kuwa msingi wa furaha yako.

Na hapo ndipo hatari huanza.

Kwa sababu hata pale kinapopaswa kuondoka, utajikuta unakishikilia kwa nguvu–hata k**a kinakuumiza, kinakugharimu, au kinakuelekeza kwenye uharibifu.

Tunaona mifano mingi katika maisha:
watu wanaong’ang’ania nafasi zilizokwisha muda wake, mahusiano yasiyowajenga n.k

Matokeo yake ni kupoteza utu, mwelekeo, na wakati mwingine, heshima yao wenyewe.

Hekima si kushik**ana na kila kitu, bali kujua kipi na wakati gani ushik**ane nacho, na wakati gani ukiachilie.

K**a msemo unavyosema:

> “Dansa mzuri si yule anayejua kudansi tu, bali anayejua muda sahihi wa kuondoka jukwaani.”

______

Elewa Hili

Ni kweli–vyeo, nafasi, vitu, na watu huleta manufaa makubwa:

- Heshima katika jamii
- Mtandao mpana wa mahusiano
- Fursa mbalimbali
- Ushawishi na umaarufu
- Kufikia karibia kila kitu

Lakini kuna upande ambao wengi hawauangalii:

- Wapo watakaokuheshimu kwa sababu ya kile ulichonacho
- Wapo watakaokukaribia kwa maslahi yao, kwa sababu ya ulichonacho

Ukijenga utambulisho wako juu ya vitu hivi, kupotea kwake kutakuacha mtupu.

Usijipoteze wewe kwa sababu umepoteza ulicho nacho.

______

Unajenga Juu ya Nini?

Mwanafalsafa hujitofautisha na wengi.

Hajengi furaha yake juu ya vitu vinavyobadilika na kuondoka
Hajitambulishi kwa vitu vinavyoweza kuondoka.

Badala yake, hujenga juu ya vitu visivyopotea kirahisi:
kusudi la maisha na huduma kwa wengine.

Cheo kinaweza kuondoka.
Nafasi inaweza kubadilika.
Vitu vinaweza kupotea.

Lakini kusudi lako haliondoki, linabadilika namna ya utekelezaji tu.

Mfano;
Ikiwa uliwahi kuongoza watu, uzoefu huo haupotei.
Unaweza usiwe tena kiongozi katika cheo, lakini unaweza kuwa mwalimu wa viongozi, mshauri, au mwongoza njia kwa wengine.

Hapo ndipo thamani yako hubaki.

Kwa mwanafalsafa:

- Nafasi ni jukwaa, si utambulisho
- Cheo ni chombo, si mwisho
- Huduma ndiyo kiini cha thamani yake
Hivyo hutumia vyote hivyo k**a vyombo vya kuhudumu na kuishi kusudi.

Ndio maana anaweza kupoteza vyote, na bado akaendelea kuwa na maana kwa wengine.

_______

Mwisho wa Yote

Mwanafalsafa hujifunza kubaki yeye; akiwa navyo, na hata asipokuwa navyo.

Kwa sababu anatambua kuwa:

- Vitu, vyeo, na nafasi huja na kuondoka
- Lakini kusudi na huduma vinaweza kuendelea milele kupitia athari anayoacha

Hivyo basi, pambana kupata mafanikio–tafuta nafasi, jenga jina, pata vitu.

Lakini usisahau kujenga kile kisichoweza kupotea:
kusudi na huduma.

Kwa sababu mwishowe,
si kile ulichokuwa nacho kitakachokutambulisha, bali ni kile ulichoweka kwenye maisha ya wengine,
na namna ulivyowagusa.

06/04/2026

WEWE NI DEREVA AMA ABIRIA WA MAISHA YAKO? #02/02

…baada ya kuona hatari ya kuishi maisha ya mazoea (life on autopilot), swali linabaki;

Unafanyaje kutoka hapo ulipo, na kuanza kuyaendesha maisha yako, na si kuwa abiria wa maisha yako?

Ukweli ni huu; hakuna mabadiliko yatakayokuja kwa bahati mbaya bali mabadiliko yote yanahitaji maamuzi ya makusudi…

…kukubali kupambania na kuyaishi maamuzi hayo siku kwa siku, mpaka yawe sehemu ya maisha yako.

Yashinde maisha ya mazoea kwa kufanyia kazi hatua hizi…

1. Jitambue na ithamini kila siku yako.

Jiulize ikiwa utaendelea kuishi hivyo, maisha yako yatakuwaje baada ya miaka mingi ijayo?

Mara zote jiulize, leo nimefanya nini? Nimepoteza muda wapi? Nini kilinitoa kwenye mstari? Kisha chukua hatua kubadilika kuwa bora.

2. Ipe siku yako mwelekeo kabla haijaanza.

Usipoichagulia siku yako itakavyoenda, mambo ya nje yataichagulia.

Kabla hujaanza siku:
- Chagua mambo machache muhimu, yanaweza kuwa matatu na zaidi,
- Yaandike,
- Amua lazima uyafanye.

3. Usisubiri hamasa au motisha bali jenga nidhamu.

Motisha itakufanya ujisikie vizuri na kuona unaweza lakini haiwezi kukupa msukumo wa kudumu,..

…jenga nidhamu binafsi ambayo itakuwa kitu cha ndani, itakusukuma kutekeleza hata k**a hujisikii, itakupa kuanza bila kusubiri na kufanya kwa mwendelezo.

4. Punguza, ondoa ama tenga muda maalumu wa vitu vinavyokuchelewesha.

Jiulize; nini kinanipotezea muda kila siku?

Simu? Mitandao? Mazungumzo yasiyo na tija?

Ukiviondoa au kuvitengea muda maalumu, utakuwa na udhibiti wa siku yako, utapata muda wa kufanya vitu vya msingi.

5. Jitengenezee mfumo wa siku.

Hata k**a hautakuwa na ratiba maalumu ya saa hadi saa…

…jiwekee mambo ya muhimu ambayo siku haipiti bila kuyafanya.

Mambo haya ni yale ambayo ni sehemu ya kusudi lako, yanayokusogeza kwenye ndoto zako, yanayokusukuma mbele, siku hadi siku.

Mfano wa mambo hayo:
- Kusoma (hata kurasa chache tu)
- Kuandika (mawazo, mipango, au kile ulichojifunza)
- Kufanya kazi kuu ya siku (deep work)
- Kujifunza kitu kipya
- Kutafakari (self-reflection)
- Matendo yanayoleta utulivu wa akili (tahajudi, kusali, tafakari za kiroho)
- Kufanya mazoezi
-kuzingatia mlo kamili
- Kupitia malengo yako

Ukishajiwekea mambo hayo, fanya kuyafanya isiwe mjadala (non-negotiable), yaani; siku haiishi hujayafanya.

Unapofanya mambo haya, hata siku ikiharibika katikati, bado unakuwa umesonga mbele.

6. Jifunze kusema hapana

Jenga thamani yako na jiwekee mipaka; usifanye kila kitu, usiende kila mahali, usipatikane kila muda, usiambatane na kila mtu,...

…jifunze kusema hapana, kwa watu na mambo yasiyo na tija, na tambua neno “HAPANA” ni sentensi kamili, inayojitosheleza, isiyohitaji utetezi wala maelezo ya ziada maana kufanya hivyo, nikuifanya “HAPANA” yako kuwa dhaifu.

7. Funga siku yako kwa tathmini

K**a ilivyo kwenye biashara, siku inapoisha lazima ufunge mahesabu, usiache siku iishe bila kutahimini,...

.kaa chini hata dakika 5 tu…
Jiulize:
- Nimefanya nini? Nimejifunza nini? Nimekosea wapi?

Hii inakupa mwanga wa nini, siku inayofuata ufanye kuwa bora zaidi.

*Hitimisho*

Maisha ya mazoea ni rahisi leo, lakini yana gharama kubwa kesho.

Rudi kwenye swali lile la awali,…

> … “K**a utaishi hivi ulivyoiishi siku ya leo, kwa miaka mitano mfululizo, utakuwa wapi?”

K**a jibu halikufurahishi, basi badilika leo.

Unaweza kuwa dereva wa maisha yako, na si abiria, ikiwa utaamua.

06/04/2026

WEWE NI DEREVA AMA ABIRIA WA MAISHA YAKO? #01/02

Hata leo kulikucha k**a vile ambavyo siku zingine huanza asubuhi.

Lakini siku yako imeishaje? Umekaa ukalitafakari hilo?

Ulipata muda wa kupanga vitu vipi ungetekeleza leo? K**a ndiyo, umetathimini vipi umefanya na kwa kiwango gani?

Na vipi je! ulipanga, lakini umejikuta unafanya vile ambavyo hukupanga kabisa?

K**a ndiyo, umechunguza, ni vipi umejikuta umefanya, na ilihali havina msaada sasa na kwa mustakabali wako?

> (Mathalani; uliamka ukajisemea, wacha niangalie kidogo simu, kisha ukajikuta umetumia masaa ukiperuzi mitandaoni…

> Uliboeka ukajisemea, acha nicheze kidogo gemu kuchangamsha akili kisha ukajikuta umetumia masaa…

> Ulijiambia tu, aah kitabu nitasoma badae, nitaandika badae, nitaomba badae, ile kazi nitaifanya badae, siku ikaisha na hujafanya kabisa, na kesho pia huenda ikawa hivyohivyo…)

Ebu pause kidogo ujiulize hili; *jinsi ulivyo iishi siku ya leo, k**a utairudia kila siku kwa miaka mitano, wapi utakuwa?*

Hivi wajua? K**a vile alivyo mtu asiyefikiri juu ya akili yake, ndivyo yalivyo maisha ya mtu asiye na utaratibu wa namna ya kuiishi siku yake!

Mtu asiye fikiri juu ya akili yake, hufikiri chochote, mawazo yake huzurura popote, hata muda ambao angepaswa amakinike, na akili yake kuwepo mahali alipo, mawazo yake humtoroka.

Vivyohivyo…

.mtu akikosa mwongozo wa siku, atafanya chochote kitakachomjia, atakachoambiwa, atakuwa na maamuzi mengi na madogomadogo pasipo kufikiri, atafanya vilevile na kuishi tabia zilezile kila siku hata k**a hazimsaidii.

Haya yanaitwa “life on autopilot”, kuishi kwa mazoea zaidi, yaani maisha ndiyo yanamwendesha mtu na sio mtu kuendesha maisha yake…

…maisha ndo yanamchagulia mtu, na si mtu kuchagua maisha yake, hapa ni pamoja na kukosa ratiba ya kwako, kukidhi matakwa, malengo na hata matarajio ya wengine…

Ukweli si kwamba watu ni wavivu ama wanapenda kuishi “on autopilot” la! Maana uko muda ambao kwa kitambo kidogo hushtuka na kufikiri juu ya namna wanavyoishi…

…kisha hubaki kujilaumu na hata kujiapiza kutoishi hivyo tena, hujiahidi kubadilika, cha ajabu bado hujikuta kwenye maisha yaleyale…

Kuishi kwa mazoea ni asili ya kihistoria ya mwanadamu, ubongo daima hujilinda na huokoa nishati hivyo hutengeneza njia rahisi na ya mkato juu ya namna akili inavyofanya kazi hata k**a si ya tija kwa mtu…

…hivyo akili itakusukuma kukwepa uwajibikaji wa makusudi, maamuzi magumu, kufikiri kwa kina…

…itabadili kila unachokifanya mara kwa mara kifanyike pasina kufikiri hata k**a si sahihi, itakuongoza kufuata mtindo wa wengi hata k**a unakupeleka chaka…

…na hatimaye hukusukuma uendelea kuatamia hali ya kujusikia vizuri (comfort zone) hata pale mabadiliko yanapohitajika...

Kuishi kwa mazoea humfanya mtu apoteze muda pasipo kujua; siku, wiki, miezi na hata miaka hupita bila cha maana kilichofanyika…

Maisha hukosa mwelekeo, na mtu huwa k**a jahazi, litwaliwalo na kila upepo, ndoto hufifia taratibu na kisha kupotea, tabia ya kuchelewesha mambo, hugeuka kughairisha mambo na kutofanya kabisa.

Na kadri miaka inavyopita maisha haya hugeukua kuwa majuto….

Nini Ufanye, Kuyashinda Maisha Haya…

23/03/2026

Wasiliana nasi: Whatsapp/normal (0693147601)

22/12/2025

NOA MSUMENO – Tabia ya Saba #01/02

Ni mara ngapi umekuwa ukifanya kazi kwa bidii lakini matokeo hayaendane na juhudi? Na wakati mwingine kulalamika kuchoka sana mwili na akili?

Ni kwa sababu hujaamua kujiboresha!

Msumeno unapotumika ni kawaida kuwa butu, hivyo ni lazima unolewe ili uendelee kufanya kazi vizuri…

…mali (asset) inahitaji kutunzwa ili iendelee kuzalisha na kupanda thamani yake…

…na ndivyo ilivyo kwa mtu pia; anahitaji kujitunza ili kuwa na ufanisi na matokeo makubwa katika maeneo yote ya maisha yake.

Hii ni tabia ya saba kwenye kitabu chake Stephen Covey; “The 7 Habits of Highly Effective People.”

Kwa mujibu wa tabia hii, mtu anapaswa kujitunza katika maeneo manne muhimu:

•Kiphizikia/Kimwili
•Kiakili
•Kiroho
•Kijamii/Kihisia

Kunoa msumeno maana yake ni kuyajali maeneo haya manne kwa usawa na kwa mwendelezo.

Kujitunza Kimwili

Hapa inamaanisha kujali mwili kwa kula vyakula sahihi, kupata muda wa kutosha wa kupumzika, na kufanya mazoezi mara kwa mara.

Mazoezi kwa ajili ya afya na kulinda mwili hayana ulazima wa kwenda gym…

…mazoezi mazuri yanaweza kufanyika nyumbani, uwanjani, fukweni na hata barabarani.

Mazoezi ya mwili yamegawanyika makundi matatu;

1. Ustahimilivu wa mwili (Endurance)
Haya husaidia mwili kutochoka haraka. Hujumuisha kutembea kwa kasi, kuendesha baiskeli, kuogelea, mchakamchaka (kukimbia).

Mtu huchukuliwa kuwa sawa kiphizikia anapoweza kupandisha mapigo ya moyo hadi angalau mapigo 100 kwa dakika na kudumisha hali hiyo kwa angalau dakika 30.
Kwa mtu mzima, mapigo ya kawaida ya moyo ni takribani 72 kwa dakika.

2. Unyumbufu wa mwili (Flexibility)
Haya ni mazoezi ya viungo yanayofanyika kabla na baada ya mazoezi makali. Husaidia kuandaa misuli, kupunguza maumivu na kuzuia asidi ya laktiki kujilimbikiza sehemu moja ya misuli.

3. Nguvu za mwili (Strength)
Haya ni mazoezi ya kuleta ukinzani au mvutano kwenye misuli, k**a push-up, pull-up, sit-ups na kunyanyua vyuma. Hujenga uimara wa mwili, nguvu na kujiamini.

Watu wengi hulalamika kukosa muda wa kufanya mazoezi, ilihali wanatoa muda mwingi kwa ajili ya wengine.

K**a unaweza kutoa saa zisizopungua 12 kwa ajili ya kazi, familia, marafiki, mitandao ya kijamii unashindwaje kutenga dakika 20 kwa ajili yako?

Tenga angalau dakika 20 kila asubuhi kabla ya majukumu au baada kwa ajili ya mazoezi, yatachaji mwili wako na hivyo kuepuka uchovu wa haraka muda wa kazi.

Mazoezi binafsi ni kwa ajili yako na ni kwa faida yako.

Karibu kundini: https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?mode=wwc

15/12/2025

Ukifanyika daraja vusha, ukiinuliwa inua, ukisaidiwa saidia, ukibarikiwa bariki...

..na haijalishi Mungu atakujalia kwa kipimo gani iwe hakikutoshelezi jifunze kutoa ili kuushinda ubinafsi na uchoyo...

..iwe kinakuzidia jifunze kupokea ili upate sababu ya kunyenyekea na kushukuru ingawaje ni kheri kutoa kuliko kupokea.

Karibu kundini: https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?mode=wwc

15/12/2025

SANAA YA USIKILIZAJI

Kwa mujibu wa Stephen Covey, kutafuta kuelewa kwanza kabla ya kueleweka, ni miongoni mwa tabia za watu wenye ufanisi wa juu.

Msingi wa tabia hii ni sanaa ya usikilizaji, ili kuelewa kwanza, unahitajika kuwa msikilizaji mzuri,...

…k**a alivyosema mwanafalsafa wa ustoa, Epictetus:
"Tunayo masikio mawili na mdomo mmoja, ili tusikilize zaidi ya tunavyoongea.”

Tatizo ni kwamba tangu utotoni tulifundishwa kuongea, kisha kusoma na kuandika tukiwa shule lakini hatukuwahi kufundishwa kusikiliza.

Ilihali usikilizaji ndio msingi wa mahusiano, uaminifu na maelewano.

HAIBA NA USIKILIZAJI

Sanaa ya usikilizaji pamoja na haiba ya mtu (uwezo wa kudhibiti hasira, utunzaji siri, kusikiliza kwa uvumilivu n.k) huwajengea hali ya usalama na imani watu wengine…

…kiasi cha kuwa wazi (kufunguka) juu ya mawazo yao, uzoefu wao na hisia zao za ndani…

…hivyo huwa rahisi kuwaelewa, kuwashauri, kufikia makubaliano ya kuridhisha pande zote na ufumbuzi wa changamoto kwa busara.

Tatizo ni kwamba watu wengi hawasikilizi ili waelewe, bali husikiliza ili wajibu.

Katika mazungumzo hungojea tu nafasi ya kujibu na hivyo kushindwa kuelewa kwa usahihi.

Kusikiliza kwa kuelewa ni kuvaa viatu vya mwingine kwa muda mfupi, yaani kusikiliza kiempathia (empathetic listening).

USIKILIZAJI WA KIEMPATHIA

Usikilizaji wa kiempathia ni kuingia kwenye mtazamo wa mwingine, ukitumia akili na moyo wako ili kuelewa kile anachosema na anachohisi.

Kwenye usikilizaji huu hupangi majibu mapema, hukatai hoja kabla haijamalizika, unatafuta kuelewa nia, hisia na hali ya mzungumzaji.

Na pia haina maana ya kukubaliana au kuhalalisha hoja ya upande mwingine bali kuelewa…

…mathalani mzazi anaweza kuelewa hoja ya mtoto, meneja hoja ya mfanyakazi, mme hoja ya mke pasipo kukubaliana…

…ni muhimu kuelewa kwanza, kwa sababu kuelewa kwanza hutengeneza mazingira ya kufikia suluhisho.

Matokeo ya usikilizaji huu ni uaminifu, ufahamu sahihi na makubaliano yenye usawa.

MBINU ZA KUSIKILIZA KIEMPATHIA

• Sikiliza sentensi zote, bila kukimbilia kujibu.
• Inapowezekana rudia kwa ufupi anachosema mzungumzaji, kwa lengo la kumhakikishia uko naye au kupata ufafanuzi zaidi.
• Usitoe ushauri mapema.
• Tambua hisia za mzungumzaji.
• Kuwa mtulivu kimwili na kiakili.

JITATHIMINI

âś“ Je, huwa unaingilia mazungumzo?
âś“ Je, huwa unachoka kusikiliza kabla ujumbe haujaisha?
âś“ Je, huwa unategemea mawazo binafsi zaidi kuliko kujenga hoja kutokana na mazungumzo wakati wa kujibu?
âś“ Je, mazungumzo kwako ni mashindano ya hoja?

K**a majibu ni ndiyo, imarisha uwezo wako wa kusikiliza.

ZINGATIA

Katika dunia ya leo yenye kelele na taarifa nyingi, uharaka, na kila mtu kutaka kusikilizwa…

…bado unaweza kujenga tabia ya kusikiliza kiempathia kwa sababu inaimarisha mahusiano, uongozi, ushawishi, na maeneo mengine ya maisha na zaidi sana ni nyenzo ya kukufanya uwe na ufanisi mkubwa.

Usipoweza kusikiliza huwezi kuelewa, na usipoelewa huwezi kuwa na ufanisi wa juu.

Karibu kundini: https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?mode=wwc

Want your school to be the top-listed School/college in Dar es Salaam?

Click here to claim your Sponsored Listing.

Location

Category

Website

Address


Dar Es Salaam