27/02/2025
Ujiji Heritage & Development Organization - UHDO
Quality Education is your Rights
27/02/2025
31/12/2024
Happy New Year, 2025
31/12/2024
Heri ya Mwaka Mpya, 2025
20/12/2024
MWANZO MGUMU, KUTOFANIKIWA AU KUFANIKIWA KWA TAMASHA KUTATEGEMEA VIGEZO VYA MTATHMINI, LAKINI HILI LA UJIJI LIMEFANIKIWA KATIKA VIWANGO VYA JUU.
Siku ya mwisho katika wiki iliyoisha, mji wa Ujiji na wakazi wake walikuwa kwenye tamati ya Tamasha la urithi wa kihistoria na Utamaduni wa mji mkongwe wa Ujiji.
Katika kuzitamatisha siku nne hizo zilizokuwa katika utaratibu wa matukio ya kiratiba, mji wa Ujiji ulipokea wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu.
Ugeni ule ulikuwa ugeni wa wachache, lakini wengi miongoni mwao walikuwa wazaliwa na wana makuzi wa mji ambao walihajiri miaka kadhaa kwa sababu mbalimbali na “Ujiji Days” k**a wengi wanavyoita ikawa ni sababu za kuwarejesha kukutana na ndugu zao.
Kwa kadiri ya ushiriki wangu nimeona iwe budi kwangu kuandika walau tathmini yangu kutokana na tamasha hili iwapo kuna kufanikiwa au kutofanikiwa kwake.
Kabla ya kuonesha hali hiyo ni vema niainishe vigezo nilivyoviweka moyoni ambavyo kwavyo walau kunaweza kunipa fursa ya madai ya kufanikiwa au kinyume chake.
Miongoni mwa vigezo muhimu kwangu ni pamoja.
1. Mji na watu wake kutambua na kushiriki Tamasha
2. Watu kufanikisha kuchangia
3. Siku zote za Tamasha kutotokea matukio ya kihalifu au jinai
4. Kutoshiriki kwa kigezo cha itikadi za kisiasa, kikabila au kimadhehebu.
5. Kutoshiriki kwa kigezo cha umri au rika
6. Watu kutoka mikoa mingine kuhudhuria tamasha
7. Watu kuonesha ari ya ushiriki wa tamasha.
8. Kutofautiana mitazamo lakini kubaki na lengo kuu la tamasha k**a mtazamo wa pamoja.
9. Kujitolea kwa watu wa mji wa Ujiji bila kuhitaji malipo.
10. Ari ya siku za Tamasha kuongezwa au mwakani kuliboresha nk
Mambo haya kumi yanaweza kutupatia natija ya kufanikiwa au kinyume chake tukiyaangaazia.
MJI NA WATU WAKE KUTAMBUA NA KUSHIRIKI TAMASHA.
Watu wa mji wa Ujiji kwa asilimia kubwa hawakuwahi kabla kulitambua Tamasha, hii ni kwa kuwa muundo wake na mijadala yake ilipitia katika makundi sogozi ya mitandao ya kijamii kwenye rununu za baadhi yetu na wenzetu, wengi katika washiriki wa mijadala hii hawakuwa watu wa mji waliopo Ujiji bali maeneo tofauti.
Katika hali hiyo utaona kuwa jambo hili lilikuwa na ushirikishwaji duni kwa watu wa Ujiji wanaoishi Ujiji, hata walipolisikia kwa kuambiwa na wenzao wa Ujiji, majibu yalikuwa ya kukatisha tamàa.
Mfano wa majibu hayo ilikuwa “wajinga ndio waliwao” “waache wapige dili” nk.
Lakini moja ya jambo jema zaidi ilikuwa wenzetu wa mikoani walipowasiliana na ndugu na jamaa zao mjini waliwauliza na kuwaelekeza ndugu na jamaa, kutopuuzia jambo hili.
Hivyo kidogo kidogo watu wakaanza kuamini kuwa jambo hili si aina ya utapeli uliozoeleka kwa baadhi ya matukio ya kabla ya jambo hili.
Ni kwa hali hiyo utaona hata walipotangaziwa kwa gari kuupita mji wote, walikuwa na utayari kuwa masiku hayo yatakuwa masiku ya Ujiji Day.
Licha ya utambuzi huo, watu bila kujali rika, dini, kabila, jinsia, cheo, ukwasi nk walifika katika viwanja vya Mzee Rashidi Mfaume Kawawa na kukaalia viti mia sita kidogo, huku wengine wakisimama na kukalia manyasi.
Ndio kusema k**a iwapo jambo hili lingefanyika kwa kushirikisha wenyeviti wa Serikali za mitaa na kuhamasisha wananchi kwenye mikutano ya mitaa, wachungaji wakawashirikisha waumini makanisani, na masheikh misikitini jambo hili lingekuwa na sura kuubwa mno kuliko tuliyoiona.
Kwa nukta hii ambayo ilitegemea kupashana habari kwa mitandao ya kijamii na rununu kupigiana na kutumiana sms, TAMASHA LA UJIJI lilifanikiwa.
WATU WENYE ASILI YA MJI KUFANIKISHA KUCHANGIA MICHANGO YA FIKRA NA PESA.
Nukta ya pili kwangu ilikuwa uchangiaji wa hiari ambao watu wa mji walishiriki.
Watu katika makundi yote yaliyokuwa yameundwa kwa ajili ya suala hili yalikuwa bize katika kutoa michango ya kifikra ya namna bora ya kuliendea jambo hili.
Kwa tabia za watu wa mji wa Ujiji, “kuzira” kwa maana ya kususia jambo ni jambo linaloenziwa na watu wengi zaidi k**a kizingishio cha kukwepa uwajibikaji kwa sababu ya kuepuka matatizo au migogoro.
Katika uandaaji wa jambo hili, ni k**a ilikuwa ni aibu kuzira, kila mmoja alionesha umahiri wa kustahmili hata k**a aliumia. Kwa maana muda fulani ingeonekana kuwa unaweka barieri kwenye jambo la mji na una kasoro fulani.
Hivyo vimbunga vya upishano wa fikra vilisababisha mizizi ya jambo hili kukita zaidi katika bongo zetu na kuliimarisha mno.
Ni wazi kuwa kuimarika kwa mizizi ya kifikra ndio kulikoimarisha pia mipango na mikakati yote iliyosababisha Tamasha hili kuwepo.
Aidha michango ya pesa kwa kila kiasi kutoka kwa kila mwana mji aliyejaaliwa kuchangia ni ishara tosha kuwa nukta hii ilionesha ubora.
Kwangu mimi sijawahi kushuhudia jambo lisilo la kidini, kisiasa kuchangiwa na watu kiasi cha zaidi ya milioni saba na jambo hilo likafikiwa na kutekelezeka bila kila mmoja kuomba ufito wake akaparate kwake.
Maana yake TAMASHA LA UJIJI lilifanikiwa
SIKU ZOTE ZA TAMASHA KUTOTOKEA MATUKIO YA JINAI.
Katika Tamasha la Mji mkongwe wa Ujiji, Tamasha lilikuwa linaanza asubuhi saa mbili na kuahirika kila saa mbili usiku.
Nyakati za Usiku Uwanja wa Kawawa ulikuwa unalindwa na Mgambo kwa ajili ya kulinda mali.
Hii sio kwamba uongozi haukuomba ulinzi wa Jeshi la Polisi, ila jeshi la polisi liliahidi kuwa watakuwa wanafanya ulinzi wa doria nyakati za usiku.
Katika masaa karibu kumi na mbili ya mchana watu wa mji walikuwa wanashiriki Tamasha lao, bila askari wala mgambo, watu hawakubishana, kutukanana, kupigana wala kuibiana.
Kila mmoja alijitahidi kuwa mwema kwa mwingine, jamii ilifanyiana kile watu wa soka husema “Fair play” ukikalia kiti kisha ukatoka kwz dharura mwingine akafika na kukaa, basi wewe ungesimama na kumpa haki na fursa ya kukaa aliyekikalia.
Tamasha lilibeba dhana ya amani na upendo usio na mipaka. Bi. Sakina Kirusha alikuwa Mwanak**ati ya maandalizi anaehusika Miundo mbinu na uwanja.
Hakuwa na wasaidizi wengi zaidi ya watoto wadogo wa mji wetu waliojitoa kumsaidia kuanzia kupanga viti, nk
Kiongozi wa Taasisi Sheikh Kabeke alibeba masahani ya chakula kuhudumia wageni. Si kwa maana ya kuwa hakukua na utaratibu, bali aliona kuwa haifai akae kwenye kiti huku wageni wetu wakiwa hawajahudumika au hajapata hakika ya huduma.
Kimsingi ni kuwa Amani ilitawala na Stahmala iliwavaa wana tamasha. Kwa uhalisia huo TAMASHA LA UJIJI lilifanikiwa
JAMII KUTOSHIRIKI KWA VIGEZO VYA MATABAKA YA KISIASA, KIKABILA AU KIMADHEHEBU.
Katika mji wa Ujiji, bila shaka utaona kuwa mambo kadhaa yamekuwa yanawachosha watu kwa kuandaa matukio ambayo yanabebwa na ushawishi wa kisiasa au madhehebu ya kidini, hivyo husababisha migawanyiko ya kiitikadi ama kisiasa au kidini.
Inapotokea hali hiyo migawanyiko hiyo huwa inaacha majeraha na madonda makubwa na baadae makovu ya mioyo ya washiriki.
Uandaaji, ushiriki na uwajibikaji wa tamasha hili haukuwa na kigezo cha siri wala cha dhahiri kinachoegemea itikadi ya kisiasa au kidini.
Hivyo mwanzo mwisho washiriki walibaki wamoja na wasio na majeraha wala makovu ya itikadi walizonazo. Mantiki hapa ni kuwa Tamasha la Ujiji lilifanikiwa.
WATU KUTOSHIRIKI KWA KIGEZO CHA UMRI AU RIKA.
Moja ya masuala yenye kuvutia zaidi ilikuwa nidhamu na adabu zinazozingatia utofauti wa rika na umri, matukio yote yaliyojitokeza siku za Tamasha yalishajiisha ushiriki wa rika na umri wowote bila mipaka.
Matukio mengi au yote yalikuwa yanaamiliana na rika zote na umri wa watu wote kuanzia watoto, vijana, watu wazima, wazee ba vikongwe. Kuwepo kwa matukio ya kinidhamu, heshima na adabu katika Tamasha hili ni alama ya kuonesha kuwa TAMASHA LA UJIJI lilifanikiwa.
WATU KUTOKA MIKOA MINGINE KUHUDHURIA TAMASHA.
Uwepo wa ndugu zetu kutoka mikoa tofauti kurejea nyumbani kwa matembezi ya mwisho wa mwaka yaliyobebwa na shajiisho la Tamasha ilikuwa ni moja ya hitaji na himizo kubwa kwa jamii ya mji wetu.
Karibu katika kila kundi sogozi, kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na ari ya kuwahimiza ndugu zetu walio nje ya mji wa Ujiji kujihimiza kurejea wao na familia zao nyumbani kwa ajili ya kuzijenga jamii kuthamini nyumbani, miongoni mwa watu waliojitokeza Tamashani ilikuwa ni pamoja na ndugu zetu Balozi Simba, kaka Fube, kaka Idd Mvano, ndugu Fadhili Mtani, ndugu M***a Kideli, kaka Hamza Mvano, Ustaadh Malilo, Sheikh Hassan Kabeke, ndugu Hussein Kikono,
Wengine ni Ndugu M***a Singwa, ndugu Nizar Kitumba, ndugu Kamana na ndugu Hanzuruni Kiroboto, ndugu Baruani Muhuza, Mkuu wa Wilaya Misungwi Mh. Samizi, Mkuu wa Wilaya ya Kipolisi Kinondoni ndugu Colle Mshauri na niridhiwe kuwataja hawa wachache katika wengi miongoni mwa mashujaa wetu.
Tendo la uthubutu wa kuacha wajibu wao wa kimaisha na kiutendaji wa kila siku na kutenga masiku machache kuyatumia kurudi nyumbani ni alama na funzo kubwa la kijamii kwa wale ambao bado hawajathubutu.
Hata hivyo ujio wao unabaki kuwa alama ya mafanikio ya Tamasha hili.
JAMII KUONESHA ARI YA KUSHIRIKI TAMASHA
Wakati Tamasha hili lilipoanza wengi ya watu katika jamii yetu walionesha kulibeza, kulidharau na wengi walikatishwa tamaa na baadhi yetu ambao kwa misuguano ya kiuandaaji na upishanaji wa mitazamo wakati wa kuliandaa Tamasha pengine walifikiri kuwa halitafanikiwa na hivyo walitoa kauli zenye zisizo na afya na zenye ukakasi kiasi watu walivunjika moyo.
Aidha misuguano iliyokuwepo kwenye kundi sogozi pia katika rununu zetu kuhusu hali halisi ya sura ya Tamasha liwe lenye kuikaribisha Serikali au k**a imeshindikana tujikaribishe na kujihudumia wenyewe ilileta sintofahamu.
Katikati ya kipindi hicho, Kamati ya Maandalizi ilidokeza haja ya kuliahirisha Tamasha kwa muktadha wa Itifaki, kilichojitokeza ndio hiki kinachozungumzwa hapa.
Jamii ilionesha ari ya ushiriki wa Tamasha, bila kujali, tulikuwa tumefika kwenye makusanyo sahihi ya pesa za kufanikisha Tamasha? Hii maana yake Jamii ilikuwa Tayari kwa Tamasha lenye sura yoyote muhimu ni Tamasha lao. Kwa hili pia Tamasha Ujiji lilifanikiwa.
KUTOFAUTIANA MITAZAMO LAKINI KUBAKI NA LENGO KUU LA TAMASHA K**A MTAZAMO WA PAMOJA.
Kwa jambo hili waliokuwa kwenye k**ati ya maandalizi watakuwa na ufahamu mkubwa sana wa hali ilivyokuwa, kwa wale wenzetu ambao walihudhuria kikao cha Tathmini ya Tamasha pale kwenye ofisi za UHDO pia watakuwa Mashahidi wa namna vikao vya Maandalizi vilivyowafanya wanak**ati kulamatana, hata hivyo badala ya kila mtu kuchukua fito yake, watu waliamua kila mmoja kukusanya fito yake kwenye ujenzi wa Tamasha. Hii maana yake Tamasha la Ujiji lilifanikiwa.
KUJITOLEA KWA WATU WA MJI WA UJIJI BILA KUHITAJI MALIPO.
Katika jambo hili nalazimika nitoe ushuhuda kuwa mama zangu kina Bi. Mombo {mama Mbufe Jaffar Kasongo}v aliniita na kunipa baadhi ya zana ili zikaoneshwe kwenye Tamasha, wapo walionipa mikeka, wapo walionipa mirage na vyungu, al muhimu ni kuwa jamii iliamua kujitoa kwa ajili ya Tamasha lao, na hadi leo siku ya tatu baada ya Tamasha Kamati ya maandalizi inaendelea kupokea taarifa za kuitwa kwenda kuchukua vifaa na zana mbalimbali majumbani zilizohitajika kwa ajili ya maonesho kwenye banda letu.
Jambo hili pia ni alama kuwa Tamasha lilifanikiwa.
ARI YA SIKU ZA TAMASHA KUONGEZWA AU MWAKANI KULIBORESHA NK
Ari hii imejitokeza katika Tamasha hili, kutokana na uhalisia kuwa kadiri siku zilivyokuwa zinasogea ndivyo ambavyo Tamasha lilionesha kunoga na kuvutia pamoja na kutimiza malengo yake kiasi hakuna mwanamji mtaalamu na asiye mtaalamu, mtawa na mlei na muumini na muasi wote kwa sifa zote, wamekuwa na ari ya kuliona Tamasha hili linafanyika kwa mara nyingine hapa Ujiji, tena likiwa na sura iliyo bora Zaidi ya iliyoonekana nyakati hizi.
Shukrani za pekee ziende awali kwa wanajamii wenyeji ambao kiuhalisia walilipokea Tamasha hili kwa dhati, SHukrani ziwaendee wanamji waliojitolea muda wao kusafiri kutoka miji tofauti kuja kushirikiana na wenzao kufanikisha suala hili.
Shukrani za dhati ziwe kwa viongozi wa Taasisi mbalimbali na Mamlaka ya Mali kale na Wizara ya Mali asili na utalii, Viongozi wa UHDO wa kanda zote, na kwa Viongozi wakuu wa Taasisi hii changa yenye wakomavu wa fikra, pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hapa UJIJI.
Hakika mmetutendea haki sisi jamii yenu.
Tukijaaliwa tutahadithia tulichokiona kuwa kina upungufu kwenye Tamasha letu.
Mwandishi wa Makala haya
Ni Chifu J. Y. Nyembo
Kasimbu Ujiji
18/12/2024
Ujiji Yetu, Fahari Yetu
Ni katika HIFADHI ya TAIFA Gombe kuangalia Sokwe
Matukio katika picha kwenye Tamsha la Urithi wa Kihistoria na Utamaduni wa Mji Mkongwe wa Ujiji 12-15 Disemba 2024
18/11/2024
Ahsante wa Kigoma hakika mmetuheshimisha. ,
17/11/2024
11/11/2024
KALUTA AMRI ABEIDI
Kukumbuka si hiyana, kwa mema aliyoata,
Alikuwa muungwana, mtu asiye matata,
Lilipaa lake jina, Simba Lumona Kaluta.
Kweli ni Simba Lumona, wa Nyakalamba Kaluta
Kweli ni Simba wa Lumona, babaye alivyomwita,
Hako atakeye kana, jina mtu lilipata,
Alikuwa ni hazina, Simba Lumona Kaluta
Kweli ni simba Lumona, wa Nyakalamba Kaluta.
Bado angali kijana, mauko yalimkuta,
Kiswahili k**a mwana, alikipaka mafuta,
Kwa juhudize twavuna, Simba Lumona Kaluta
Kweli ni simba Lumona. wa Nyakalamba Kaluta
Alihaha kila kona, akaasisi UKUTA,
Umoja akausana, ushairi ukavuta,
Tuta kukumbuka sana, Simba Lumuna Kaluta,
Kweli ni Simba Lumona, wa Nyakalamba Kaluta
Tungo alipenda sana, na sheria akaleta
Zikasomwa Kila kona, kwa hojaze zikapita,
Kwazo Sasa twajivuna, Simba Lumona Kaluta,
Kweli ni Simba Lumona, wa Nyakalamba Kaluta.
Lugha imekuwa pana, Afirika limepita,
Yatumika hata China, sasa haina matata
Kiswahili kimenona, Simba Lumona kaluta.
Kweli ni simba Lumona, wa Nyakalamba Kalutu,
Kwa kila alilonena, lugha aliifumbata,
Mashairi kayasana, wanati yakawavuta,
Na wala hakujivuna, Simba Lumona Kaluta.
Kweli ni simba Lumona, wa Nyakalamba Kaluta.
Amnusuru Rabana, motoni asende tota,
Amali alizo sana, hako awezaye futa,
Litabaki lake jina, Simba Lumona Kaluta,
Kweli ni Simba Lumona, wa Nyakalamba Kaluta.
MKANYAJI
Hamis Ally Kisamvu
0715311590/0784311590
[email protected]
Baitu shi'ri
Mabibo - Dar es salaa
Click here to claim your Sponsored Listing.
Location
Category
Telephone
Address
Shekilango Ubungo
Dar Es Salaam
255