29/05/2026
🎓 SEPTEMBER INTAKE 2026/2027 🎓
Dirisha la Udahili limefunguliwa rasmi tarehe 28/05/2026.
Tunawakaribisha wanafunzi wote wa ngazi ya Certificate na Diploma kujiunga nasi katika kozi mbalimbali zitolewazo na chuo.
✅ Maombi yote yanafanyika kwa njia ya mtandao kupitia:
👉 olap.eastc.ac.tz
🌐 Tembelea tovuti yetu kwa taarifa zaidi:
👉 www.eastc.ac.tz
📞 Mawasiliano:
Simu: +255 713 988 952/0757539836/0759 042 143
Barua pepe: [email protected]
20/05/2026
DKT.KATUNZI ATEMBELEA MAFUNZO YA TAKWIMU YANAYOENDELEA NCHINI ZIMBABWE.
Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Dkt. Tumaini Katunzi, ametembelea mafunzo yanayoendelea nchini Zimbabwe yanayowahusisha maafisa wanaofanya kazi katika mifumo ya kitaifa ya takwimu nchini humo.
Mafunzo hayo ya “National R Training in SADC Member States”, yanatolewa na wahadhiri kutoka Chuo cha Takwimu kwa kushirikiana na SADC, yakiwa na lengo la kuwaongezea ujuzi maafisa wa mifumo ya kitaifa ya takwimu ili waweze kuchakata, kuchambua na kuzalisha takwimu rasmi kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo mara baada ya kuwasili, Dkt. Katunzi amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa na manufaa makubwa iwapo washiriki watatumia maarifa watakayoyapata katika shughuli zao za kila siku za uzalishaji wa takwimu rasmi.
Aidha, amewahimiza washiriki kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili waweze kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika kuimarisha mifumo ya takwimu na ubora wa takwimu katika nchi zao.
12/05/2026
Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Dkt. Tumaini Katunzi, leo Mei 12, 2026 alipokea ugeni kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia — Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Kitaifa, iliyoongozwa na Kaimu Mwenyekiti, Prof. Msanjila.
Katika ziara hiyo, wajumbe walipata fursa ya kusikiliza wasilisho kuhusu hatua za utekelezaji wa mradi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa jengo la taaluma pamoja na ukarabati wa hosteli.
Kamati ilipongeza maendeleo yaliyofikiwa na kusisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za ujenzi ili kuhakikisha mkandarasi anakamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa.
Aidha, wajumbe walitembelea eneo la mradi kujionea maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi huo.
11/05/2026
Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC),kinaendelea kutoa mafunzo kwa nchi wanachama wa SADC kupitia programu ya “National R Training in SADC Member States” nchini Zimbabwe. Zimbabwe imekuwa nchi ya pili kunufaika na mafunzo hayo baada ya Eswatini.
Mafunzo hayo yanafanyika jijini Harare kuanzia tarehe 11 hadi 22 Mei 2026, na yamefunguliwa rasmi leo na Bw. Mukhavi, Mkurugenzi wa Takwimu za Kidemografia na Kijamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Zimbabwe.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, mwakilishi wa SADC Bi. Zarafenosoa Ruth amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo katika kuzijengea uwezo nchi wanachama kuzalisha na kuchakata takwimu bora zitakazosaidia tathmini ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa niaba ya Chuo cha Takwimu, wawezeshaji wa mafunzo hayo Edwin Magoti na Leguma Bakari wameishukuru SADC kwa kuwezesha programu hiyo, huku wakiwataka washiriki kushiriki kikamilifu ili kufanikisha malengo ya mafunzo hayo.
09/05/2026
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri pamoja na Menejimenti ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) walitunukiwa vyeti baada ya kuhitimisha mafunzo ya siku mbili kuhusu Corporate Governance and Capacity Building. Mafunzo hayo yalifanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere (Mwalimu Julius Nyerere Leadership School) kilichopo Kihaba, kuanzia tarehe 07 hadi 08 Mei 2026.
08/05/2026
Mafunzo ya Utawala Bora wa Taasisi na Kujengewa uwezo kwa Wajumbe wa Bodi ya Ushauri na Timu ya Menejimenti EASTC.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Prof. Ahmed Mohammed Ame, alifungua rasmi Mafunzo ya Utawala Bora wa Taasisi na kujengewa uwezo kwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri na Timu ya Menejimenti, yaliyofanyika katika Chuo cha Mwalimu Julius Nyerere Leadership School, kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani, tarehe 07–08 Mei 2026.
Mafunzo hayo yameendeshwa na The Institute of Directors in Tanzania kwa lengo la kuimarisha uongozi, uwajibikaji, na ubora wa taasisi kupitia maarifa ya vitendo na uzoefu wa kitaalamu.
05/05/2026
KIKAO CHA WADAU CHA KUHUSISHA NA KUANZISHA MITAALA
Kaimu Mkuu wa Chuo, Dkt. Indiael Daniel Kaaya, ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, alifungua kikao cha wadau kilicholenga kuhusisha wadau katika mchakato wa kuanzisha na kuboresha mitaala ya chuo. Kikao hicho kinafanyika kuanzia Mei 04–06, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa EASTC.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kaaya aliwahimiza wataalamu kutoka EASTC kutumia fursa hiyo kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau ili kuboresha mitaala ya chuo na kuhakikisha inaendana na matakwa ya NACTVET pamoja na mahitaji ya soko la ajira.
Aidha, alieleza mitaala nane (8) itafanyiwa mapitio na kuhuishwa, huku mitaala mitatu (3) mipya ikitarajiwa kutengenezwa na kuanzishwa katika mwaka wa masomo 2026/2027.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi, Wizara, Halmashauri, Vyuo,Makampuni , Walimu pamoja na Wanafunzi wa EASTC.
01/05/2026
MAADHIMISHO YA MEI MOSI 2026.
Watumishi wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC),Kampasi ya Dar es Salaam na Dodoma wameungana na Wafanyakazi wote Duniani leo Mei 1, 2026, kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi).
Maadhimisho hayo kwa ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam yamefanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na Mkoa wa Dodoma yamefanyika katika Viwanja vya Jamhuri yakihudhuriwa na Viongozi mbalimbali pamoja na Wafanyakazi kutoka sekta tofauti.
Kauli Mbiu “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050”.