23/04/2021
Assalam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah ( SW )
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
Leo tutaendelea na fadhila za kumi la pili la mwezi mtukufu wa Ramadhani, ikiwa ni muendelezo wa darsa liliopita.
(2) KUMI LA MSAMAHA
Kumi la pili la mwezi wa Ramadhani ni masiku yaliyo bora zaidi kwa waumini kutokana na kuletewa karibu fursa ya kusamehewa makosa yetu yaliyotangulia.
Bila shaka Mwenyezi Mungu mtukufu ndiye mwenye kusifika kwa sifa ya kuwasamehe viumbe wake na amelieleza hilo katika aya nyingi ndani ya kitabu chake kitukufu.
Anasema Mwenyezi Mungu katika surat Nnajim 32
{ Hakika ya mola wako ni mwingi wa msamaha }
Bila ya shaka yoyote ile tunapata kuona ukubwa wa msamaha wa Allah kwa viumbe wake na amewataka wajitahidi kuomba msamaha zaidi kwakuwa yeye hatokuwa mchoyo wa kuwasamehe.
Hivyo tunatakiwa kuongeza bidii katika hili kumi la pili kwa kufanya ibada kwa wingi kutoa sadaka kwa wenye mahitajio pia kuwa karibu na mayatima na kuwatembelea wagonjwa na kuwasaidia katika matatizo waliyonayo huku tukiomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kutokana na matendo tuliyoyafanya kwa kusahau au kwa kujua ubaya wake au kwa kutokujua.
Anasema Mtume Muhammad ( saw )
"Hakika Mwenyezi Mungu hachoki kutoa msamaha ikiwa watu hawatoacha kumuomba msamaha"
Hivyo basi tulitumie vyema hili kumi la pili katika kuhakikisha tunafutiwa dhambi zetu zote.
Allah atujaalie kuwa miongoni mwa viumbe vyake vinavyomtaka msamaha.
Itaendelea...!
Tumuombe Allah atukubalie funga zetu na atujaalie mwisho mwema.
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)
20/04/2021
Assalam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah ( SW )
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
Katika muendelezo wa zile darsa zetu fupi za mwezi wa Ramadhani, leo tutaangalia mgawanyiko wa masiku katika mwezi huu mtukufu.
Miongoni mwa mafunzo tuliyoyapata kutoka kwa mtume wetu ni kuwa masiku ya mwezi wa Ramadhani yamegawanywa katika sehemu tatu k**a ifuatavyo:-
(1) Rahma / (Rehema)
(2) Magh'fira / ( Msamaha )
(3) It'qu minannari/ ( Kuachwa huru kutokana na moto ).
Vigawanyo hivi vitatu tumevipata kupitia hadithi ya Mtume Muhammad ( saw ) pale alivyosema.
( Mwanzo wa mwezi wa Ramadhani ni Rehema, kati ni Msamaha na mwisho wake ni Kuachwa huru kutokana na moto )
Hivyo ni bahati kubwa sana kwetu kwa kulidiriki hili kumi la kwanza la Rehema, na mazungumzo yetu yataanzia hapo na kumalizia na yaliyobakia.
(1) KUMI LA REHEMA
Katika kulielezea kumi hili la kwanza la mwezi wa Ramadhani hatuwezi kuacha kutaja fadhila zake ambazo ameziweka Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake, fadhila hizo zikitawaliwa na tukio zima la kuwapatia rehema viumbe vyake dhaifu k**a ilivyotangulia kutajwa jambo hilo katika Hadithi ya Mtume wake mtukufu.
Mwenyezi Mungu ndiye anayesifika kwa sifa ya kuwa ( Rahiim ) kwa viumbe vyake na jambo hilo lipo wazi katika maisha yetu ya kila siku hata katika ibada zetu
kwani huruma yake imefanya suala zima la maisha ya mwanadamu kuwa na nyenzo zote anazozihitajia ili aweze kuishi katika dunia hii.
Rehema ya Mwenyezi Mungu katika mwezi huu wa Ramadhani imezidia mno kulinganisha na masiku ya miezi mingine, na ameihusisha rehema hiyo katika masiku maalum ambayo yanaanzia tarehe moja Ramadhani mpaka tarehe kumi ( masiku kumi ya mwanzo ).
Basi inatakikana kwa kila muumini atumie fursa hii ili apokee rehema za mola wake hasa katika haya masiku kumi ya mwanzo, na wala hatoweza kufanikisha jambo hilo ila kwa kuwafanyia huruma watu pia kuwahurumia viumbe wengine na kuwafanyia wema.
Anasema Mtume wa Muhammad ( saw )
""Hakika anawarehemu Mwenyezi Mungu katika viumbe wake wale wanao warehemu wenzao".
Basi kuwafanyia huruma wenzetu ndio njia pekee na ya haraka katika kupata rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Njia nyingine ya kutupeleka katika rehema za Allah ni kuwafanyia wema Masikini na Mafukara kwa kuwapatia aina tofauti za misaada ikiwemo hata kuwafuturisha.
Anasema Mtume ( saw )
" Wafanyieni huruma waliopo katika dunia ili awapatie rehema aliyeko mbinguni".
Itaendelea inshaallah...!
19/04/2021
Assalam Alaykum
Shukran zote ni za Allah ( SW )
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
Katika kuendelea na darsa zetu za Ramadhani, leo tutaangalia hoja ingine ya wanaodai kuwa Ibada ya Funga ni Adhabu.
(3) Je funga ina madhara yoyote kwa mfungaji..?
Tumetangulia kuona hoja za wasioupenda uislam katika kutia dosari Ibada yetu tukufu kwa kuleta madai yasiyo na ukweli wowote na wakafikia kusema kuwa ibada ya funga ni adhabu kwa waislam kwani ina madhara ya kiafya.
Katika kujibu tuhuma hii tunaweza kuwarudisha nyuma kidogo na kuwakumbusha aya ile ile ya 183 katika surat Baqara ambayo Mwenyezi Mungu ameifaradhishia funga kwa waislam kwani imeweka wazi huruma yake kwa viumbe wake na kuweka ruhusa maalum kwa watu waliokuwa na dharura.
Tumeliweka wazi jambo hilo katika somo lililopita na kuonyesha watu waliopewa nafasi ya kula mwezi wa Ramadhani na hukumu ya kila mmoja kwa mujibu wa tatizo lake.
Baada ya utangulizi huo sasa tunapenda kuwajibu hoja yao dhaifu kwa kuwaambia kwamba funga ya Ramadhani haina tatizo lolote katika afya ya mwanaadam, na ikitokea mtu ana matatizo ambayo hawezi kuhimili Ibada hii ya funga basi ameshawekewa ruhusa na Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitukufu au kuwekewa uchambuzi zaidi katika Hadithi za Mtume wake (saw).
Ikitokea Muislam yeyote akatambua hali yake ya afya haipo vizuri basi atatakiwa aache kufunga na ajitibu kwanza kisha atakuja kulipa hiyo funga akiwa yupo mzima wa afya kamili, na ikitokea amejilazimisha na akapata madhara ya kupelekea kifo chake hali ya kuwa alitambua basi atahukumiwa kwa kitendo cha kujisababishia kifo, kwani sheria imempa nafasi mpaka mama anayenyonyesha akiona hayupo na uwezo kuhimili funga kwa ajili ya nafsi yake au mtoto anaye nyonyesha basi aache kufunga.
Anasema Mtume Muhammad (saw)
( Hakuna Madhara wala Kujidhuru )
Katika upande wa pili funga imethibitishwa na madaktari bingwa kuwa ni msingi mkubwa wa kutengeneza afya ya mwanaadam na wamekiri kuwa ukiachana na faida ya kiroho aliyoitaja Mwenyezi Mungu pia Funga ina faida kubwa kwa afya ya mwanadamu.
Anasema mtume Muhammad (saw)
( Fungeni Mtapata Afya )
Tumuombe Allah atujaalie funga zenye kukubaliwa na atupatie mwisho mwema.
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
( Kiwalani Minazi Mirefu )
18/04/2021
Assalam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah ( SW )
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
Katika kuendelea na darsa zetu fupi za Ramadhani, leo tutaendelea pale tulipoishia katika somo lililopita...!
(2) Je funga ni ibada au adhabu..???
...Pia funga sio adhabu k**a wanavyodai katika hoja yao wanayoleta ili kuitia dosari ibada hii tukufu.
Katika kuliweka wazi jambo hilo tunaona kuwa Mwenyezi Mungu ametoa ruhusa ya kula katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa watu wote wenye dharura na kutakiwa kulipa hiyo funga katika masiku yajayo.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika surat Baqara 185
{ ...Na yule atakayekuwa mgonjwa au yupo safirini basi na alipe hiyo swaum katika masiku mengine, Hakika anawatakia Mwenyezi Mungu wepesi na wala hawatakii uzito..}
Aya hii inaweka wazi huruma ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake, ametambua kuwa katika sisi wapo watakaokuwa na udhaifu wa aina tofauti hali ambayo itawafanya washindwe kutekeleza ibada hii tukufu, akatoa ruhusa kwa watu hao kula ndani ya mwezi wa Ramadhani na kuweza kulipa hiyo funga katika masiku mengine.
Huu ndio uislamu na hayo ndiyo malezi ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake, anawaambia wazi kuwa anawatakia wepesi katika Ibada zao na wala haitajii kuwapa uzito wa aina yoyote.
Wapo wapi wale wanaodai kuwa ibada ya funga ni adhabu...!!! Je wamekisoma vizuri kitabu cha Allah na kukielewa..!!! Je wanajua kuwa sheria za kiislam zimewapa nafasi watu wa aina zote kuweza kutekeleza ibada kwa mujibu wa hali zao za kiafya na kiuchumi..?
Baada ya kuyasema hayo machache katika mengi yanayovunja hoja zao dhaifu, tunasema ya kwamba Ibada ya funga sio adhabu kwa waislamu ila ni fursa na nafasi ya kujisogeza zaidi kwa mola wao mlezi.
Katika kulithibitisha hilo hebu tuangalie sheria ya kiislamu ni jinsi gani ilivyoweka misingi sahihi ya funga na kuwapa ruhusa ya kula wenye dharura mbalimbali kwa kujali hali zao za kiafya za kila siku k**a ifuatavyo:-
>Walioruhusiwa kula na kulipa funga baadae.
(1) Mgonjwa
(2) Msafiri
(3) Mwenye Hedhi au Nifasi
>Hawatofunga ila wanaweza kulipa fidia ikiwa wana uwezo
(1) Mgonjwa mwenye maradhi ya kudumu
(2) Mzee
>Wasiolazima kufunga (labda kwa kujifunza)
(1) Watoto wasiofikia baleghe.
Kwa hali hii vipi mtu aseme eti funga ni Adhabu, labda awe na upungufu wa akili kichwani.
Itaendelea..!!!
Tumuombe Allah atujaalie funga zenye kukubaliwa na atupatie mwisho mwema.
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)
17/04/2021
Assalaam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah ( SW )
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
Katika kuendelea na darsa zetu fupi za Ramadhani leo tutagusia nukta ya pili katika kuwajibu wale wanaodai kuwa Ibada ya funga ni Adhabu.
(2) Je Ibada ya funga ni adhabu?
Katika darsa lililopita tuliangalia Asili ya funga na tukapata faida ya kuwa funga ni ibada iliyokuwepo katika zama za watu walitangulia.
Swali lililopo mbele yetu linahitaji majibu sahihi ili kuweka fikra na akili za wengi katika ufahamu ulio sawa.
Hoja yao dhaifu ya kudai kuwa waislam wanakaa na njaa ikiwa ni adhabu kutoka kwa Mungu wao, kwani hakuna ibada inayowekwa ndani yake kukawa na mateso....!!!
Katika kujibu hoja yao hii tunawaambia kuwa dini ya uislamu imejengwa juu ya nguzo tano madhubuti, nazo ni:-
Shahada, Swala, Zaka, Funga na Hijja.
hivyo Funga ya Ramadhani ni nguzo ya nne katika nguzo za uislam na haiwezekani kuthibiti uislamu wa mtu yoyote kwa kupinga nguzo yoyote katika hizo nguzo tano zilizotajwa hapo juu.
Baada ya utangulizi huo tutaona kuwa wapingaji wa ibada ya Funga sio waislamu na wala hawaujui undani wa dini ya uislamu katika ufahamu ulio sahihi, hivyo acha tuwaoneshe hekma ya Mwenyezi Mungu kuileta hii funga kwetu na kuifanya kuwa ni lazima kwa kila mtu aliyekidhi vigezo.
Anaweka wazi Mwenyezi Mungu Mtukufu lengo la Funga mwishoni mwa aya iliyolazimisha swaum.
{ Enyi mulioamini mumelazimishwa kufunga k**a walivyolazimishwa watu waliokuwa kabla yenu, ili mupate kuwa wachamungu } surat Baqara 183
Kupitia aya hii iliyokuja kuleta ulazima wa kufunga tunaona mwisho wake kumeelezwa lengo la sisi kufunga nalo ni lengo letu la kuumbwa na Mwenyezi Mungu k**a anavyosema katika surat dhariyaat 56
{ Sijawaumba Majini na Watu isipokuwa kwa ajili ya kuniabudu }
Hivyo hekima ya Mwenyezi Mungu kutuletea Funga ni kutupatia njia ya mkato ya kufikia malengo ya kuumbwa kwetu kwani faida ya swaumu iliyokubwa zaidi ni kuupata uchamungu na kutimiza lile lengo la kuumbwa kwetu na Allah.
Pia Funga sio adhabu k**a wanavyodai katika hoja yao wanayoleta ili kuitia dosari ibada hii tukufu, ..............!!!!
Tutaendelea Inshaallah..!!
Tumuombe Allah atujaalie funga zenye kukubaliwa na atupatie mwisho mwema.
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)
16/04/2021
Assalaam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah (SW)
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
Je Swaumu ni Ibada au Adhabu kwetu...??
Katika kuendelea na darsa zetu fupi za Ramadhani, leo nimependelea kuweka wazi swali linalopita katika akili za watu wengi kuhusu ulazima wa Funga ya Ramadhani.
Kwa hakika kumekuwa na kundi la watu wasiokuwa waislam wanaopotosha uhalisia wa Ibada ya Funga ya Ramadhani na kudai kuwa ni adhabu na hakuna heri yoyote wanayoipata waislam kupitia funga hiyo.
Wanatilia nguvu maneno yao kwa madai yasiyokuwa na ukweli wowote isipokuwa ni chuki na uadui wa wazi dhidi ya ibada zinazofanywa na wafuasi wa dini ya Kiislam.
Moja ya hoja zao ambazo ni dhaifu mno ni kwamba eti Funga ni adhabu kwa mwanadamu kwani hakuna ibada ya kuwafanya watu wakae na njaa hali ambayo huja ikawa ni tatizo kwa afya zao.
Katika kujibu hoja yao hii dhaifu lazima tuangalie asili ya funga, je imeanzia kwa watu wa Mtume Muhammad (saw) au ilikuwepo kwa watu waliotangulia kabla yetu, pia tuangalie je ni kweli Swaumu ni adhabu au inaviashiria vya kuwatesa waislam kwa kulazimishwa kufunga, mwisho kabisa tuangalie je kuna madhara yoyote kwa wenye kufunga k**a wanavyodai watu wasioupenda uislamu.
(1) Asili ya funga.
Funga ya Ramadhani imefaradhishwa kwa watu wa Mtume Muhammad ( saw ) ikiwa ni muendelezo wa aina mbalimbali za Funga ambazo walifaradhishiwa watu wa Mitume iliyotangulia.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika surat Baqara (183)
{ Enyi wale mulioamini, Mumefaradhishiwa funga k**a walivyofaradhishiwa watu walikuwa kabla yenu ili mupate uchamungu }
Kupitia aya hii tukufu tunapata jibu la maadui wa Uislamu ambao wamekuwa ni wenye kuzitia dosari ibada zetu bila ya kuwa na uelewa sahihi wa kile wanachokikosoa.
Ameweka wazi Mwenyezi Mungu Mtukufu kupitia aya hii kuwa jambo la kufunga halijaanza kwa watu wa Mtume Muhammad (saw ) bali ni jambo lililorithiwa kutoka kwa watu wa zama zilizopita.
Hivyo basi, tunawapa ufahamu sahihi kuhusiana na funga kuwa ni IBADA iliyofanywa na watu wa mitume tofauti, ila tofauti ipo katika sharti na nguzo za ufungaji ndio zinazobadilika.
Itaendelea...!!!!
Tumuombe Allah atujaalie funga zenye kukubaliwa na atupatie mwisho mwema.
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)
15/04/2021
Assalam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah (SW)
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
FADHILA ZA SWAUM
(sehemu ya tatu)
(3) Katika mambo yaliyoifanya funga ya Ramadhani kuwa ni bora na fadhila zake kutokuwa na ukomo ni:-
Funga ya Ramadhani imefaradhishwa katika mwezi ulio bora zaidi ya miezi yote.
(1) Ramadhani Mwezi wa Qur an,
Katika heri kubwa iliyopatikana ndani ya mwezi huu ni kuteremka kwa kitabu kitukufu ndani yake, kwani imeteremshwa Qur an yote kutoka katika Lauhul Mahfuudh mpaka katika Baytul Izza katika Mbingu ya dunia katika usiku mmoja, kisha ikawa inashuka kidogo kidogo kwa Mtume Muhammad (saw) kwa muda wa miaka (23),
Mwanzo wa kushuka Qur an ilikuwa ni katika usiku wa cheo (Lailatul Qadr).
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu.
{ Hakika tumeiteremsha Qur an katika usiku wa cheo } surat Qadr 1.
(2) Ramadhani mwezi uliofaradhishwa funga,
Katika dini ya kiislam kuna aina nyingi za funga lakini funga ya mwezi wa Ramadhani imekuwa ni lazima kwa kila mtu aliyekidhi vigezo vya kufunga.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu.
{ Yule atakaye udiriki mwezi wa Ramadhani basi ni lazima afunge } surat Baqara 185.
(3) Ramadhani ni mwezi ambao ndani yake kuna Usiku mmoja ambao ibada ndani ya usiku huo ni bora zaidi ya ibada katika miezi elfu moja (1000).
Kwa hesabu za kawaida ni kwamba usiku ulipo ndani ya mwezi wa Ramadhani unazidia takribani miaka (83) ya maisha ya binaadam.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu.
{ Usiku wa cheo ni bora kuliko miezi elfu moja } surat Qadr 3.
Aidha, mwezi mtukufu wa Ramadhani unawaweka karibu mno watu wema na mola wao pia huwaweka mbali watu waovu na Mwenyezi Mungu,
Kwani pindi unapoingia mwezi wa Ramadhani hufungwa mashaitwani kwa minyororo pia hufungwa milango ya moto bila kusahau milango ya pepo hufunguliwa na hakuna cha kumpoteza mtu isipokuwa ni nafsi yake pekee.
Tumuombe Allah atujaalie funga zenye kukubaliwa na atupatie mwisho mwema.
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)
14/04/2021
Assalam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah (SW)
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
FADHILA ZA SWAUMU
(sehemu ya pili)
(2) Miongoni mwa fadhila za Swaumu kwa mfungaji ni kupata Kinga ya nafsi kutokana na matamanio ya Dunia, pia kuwa kinga ya adhabu ya Mwenyezi Mungu Akhera, pia ni ngome iliyo madhubuti kutokana na vitimbi vya Mashetani waliolaaniwa, kwani anasema Mtume Muhammad ( saw )
"Swaumu ni Kinga".
Hivyo swaumu ni chombo chenye kuhifadhi nafsi kutokana na vishawishi vya mashaitwani.
Aidha Funga ni chombo pekee chenye kuiadabisha nafsi na kuutuliza ulimi na viungo vya mfungaji kutokana na maneno mabaya au kuyafanyia kazi, pia funga ni yenye kuitia subira nafsi kutokana na maudhi ya watu.
Anasema Mtume Muhammad (saw)
"Pindi anapokuwa amefunga mmoja wenu basi asifanye mambo ya kipuuzi wala ujinga, na ikitokea mtu amemtukana au amempiga basi amwambie kuwa mimi nimefunga."
Katika hadithi hii tunaona kwa uwazi ulio mkubwa kuwa kitendo cha mtu kufunga kinamfanya awe ni mwenye kukatazika na mambo yasiyofaa, na katika kulitilia mkazo jambo hilo anasema Mtume Muhammad (saw)
"Mtu ambaye hajaacha maneno ya uovu (uongo) na pia kuyafanyia kazi, basi Mwenyezi Mungu hana haja na kuacha kwake kula na kunywa."
Tumuombe Allah atujaalie Funga zenye kukubaliwa na pia atupatie Mwisho mwema.
Itaendelea inshaallah...!
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)
13/04/2021
Assalam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah (SW)
Rehema zimfikie Mtume wake ( SAW)
Hatuna budi kushukuru kwa kupewa nafasi hii ya kuudiriki tena mwezi mtukufu ambao ndani yake ndio kimeshuka kitabu kitukufu cha Qur an, hivyo kuufanya mwezi huu kuwa na usiku mmoja wenye ubora zaidi ya miezi elfu moja.
Tumependelea kuweka darsa fupi za fadhila za mwezi wa Ramadhani kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa huu mwezi ili tukumbushane yale mambo muhimu na tuyafanyie kazi ili tufikie katika darja la uchamungu, kwani huu mwezi ni karakana ya kutengeneza maisha yetu ya kila siku.
Leo tutaanza na fadhila za mwezi huu mtukufu.
Hakika fadhila za Swaumu( Funga ya Ramadhani ) na siri zilizopo ndani yake hazina ukomo wa kudhidhibiti. Miongoni mwa fadhila hizo ni k**a ifuatavyo:-
(1) Anasema Mtume Muhammad (saw) "Mtu mwenye kufunga swaumu ya Ramadhani hali ya kuwa ni mwenye imani, na huku akiamini kuwa atalipwa na Mwenyezi Mungu, basi atasamehewa mtu huyo yale aliyoyatanguliza katika madhambi yake".
Bila shaka haya ni malipo makubwa kwetu kutoka kwa Mola wetu mlezi ikiwa tutafata sharti na nguzo za kufunga.
Pia bila ya kusahau kuwa malipo ya kila jambo la heri ( Ibada ) huongezwa kwa Jema Moja kulipwa mara KUMI zaidi mpaka mara MIA SABA na zaidi, anasema Mtume Muhammad (saw) " Matendo yote ya wanadamu hulipwa kwa ziada, jema moja huongezwa mara kumi mfano wake mpaka hufika ziada ya mara mia saba na zaidi. Kisha akasema isipokuwa malipo ya Swaumu kwani anasema Mwenyezi Mungu mtukufu kwamba
( "Hakika swaum ninaisimamia mimi mwenyewe na hakika mimi ndie ninaye jua malipo yake" ).
Hapa tutaona ubora wa swaum na jinsi gani Mwenyezi Mungu ameipa upekee zaidi ya ibada nyingine, na jambo hilo ni zawadi kwa wenye moyo safi na imani thabiti, kwani Mwenyezi Mungu ameliweka wazi hilo pale alipoeleza sababu ya kusimamia malipo ya swaum pale aliposema
( "Anaacha mtu matamanio yake na kuacha chakula chake kwa ajili yangu" )
Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie Funga zenye kukubaliwa na atupatie mwisho mwema...!
Itaendelea Inshaallah...!!!
Imeandaliwa na :-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)
24/07/2017
Assalaam alaykum
HAYA الحياء
Sehemu ya tano.
Anasema mtume MUHAMMAD (s.a.w) لو كان الحياء رجلاً لكان رجلاً صالحاً، ولو كان الفحش رجلاً لكان رجلاً سوءاً.
" lau HAYA ingelikuwa ni mtu, basi angekuwa mtu mzuri mno. Na lau uovu ungelikuwa ni mtu, basi angekuwa mtu mbaya sana.( twabraniyy).
Ina HAYA sehemu ambazo imependekezwa zaidi.
(1) haya ktk mazungumzo
Inatakiwa kwa mwanaadam kitakasike kinywa chake tokana na maneno machafu, ujiepushe ulimi wake na dosari, ajiweke mbali na kutaja sehemu za siri (العورات ). Kwani ktk adabu iliyo mbaya kabisa kumtoka mtu maneno machafu bila ya kujari sehemu alipo na athari zake.
Na miongon mwa HAYA ktk mazungumzo ni kufanya uchache maneno ktk kikazi (mkusanyiko), kwani baadhi ya watu hawaoni haya kuzua zua habari na kipiga porojo ktk mkusanyiko wa watu, na ikawa sababu ya kuwachosha watu kwa urefu wa mazungumzo hayo, na uislam umekataza tabia ya aina hii.
Anasema mtume MUHAMMAD إن الله يبغض البليغ من الرجال.........
"hakika ALLAH anamchukia mtu mwenye kuzidisha zidisha maneno............" (tirmidhiyy).
Siri ya kuchukiwa mtu wa tabia hii, kwamba habari zao haziepukani na uzidishwaji( uongo) na hali zao zinajaa kujionyesha ( riyaa), na wamejawa na ushindani wa kuvuta makundi ya watu. Sasa ikawa dawa ya ugonjwa huu ni kuwa na HAYA.
Allah atujaalie mwisho mwema
Tutaendelea inshaAllah.
23/07/2017
Assalaam alaykum
HAYA. الحياء
Sehemu ya nne.
Mtume Muhammad (s.a.w) anasema :- " hakika mwenyezi mungu mtukufu pindi anapotaka kumuangamiza mja, basi huondosha kwa mtu huyo *HAYA*. Na pindi atakapokosa HAYA, basi haitomfikia yy ispokuwa machukivu na pindi yakimfikia machukivu basi huondosha ALLAH kwa mtu huyo uaminifu, na akiondoshewa uaminifu haitomfikia mtu huyo ispokuwa ni kufanya hiyana, na na atakapokuwa mfanya hiyana, ALLAH atamuondoshea rahma na hapo sasa atabakia mtu huyo ni mwenye kulaaniwa. Na pindi atakapokuwa mwenye kulaaniwa, basi ALLAH anamuondoshea mtu huyo alama za uislam. (Ibn maaja)
Na utaratibu huu wa ndani kabisa ktk kuyaeleza maradhi ya nafsi na na kufatiliwa na athari zake, vp atasalimika kutoka ktk tatizo moja mpk lingine ambalo ni kubwa zaidi ubaya wake.
Pindi mtu anapo ondoa pazia la HAYA ktk uso wake na akawa hayakagui matendo yake, na haogopi ktk tabia zake lawama ya yeyote, akawa anawaudhi watu kwa kutumia nguvu zake, basi mfano wa mtu k**a huyu hatopata moyo wa kiumbe yeyote wa kuweza kumuonea huruma na atakuwa anapandikiza chuki ktk mioyo ya watu na kuzikuza dhidi yake.
Mwanadamu akiwa na sifa hizi hatoaminiwa na yeyote yule, vp atapata kuaminiwa ktk mali ambayo haogopi kuila, au ktk cheo ambacho aoni haya kukifedhehesha, au ktk ahadi ambayo haon haya kuihalifu, au ktk majukumu ambayo hashindwi kuyapindukia, au ktk bidhaa ambazo haepukani na kuzifanyia ghushi ndani yake...
Allah atuepushe na mtihan huu ..aaaaamin
Inshaa ALLAH tutaendelea....!!!
22/07/2017
Assalaam alaykum
HAYA. الحياء
Sehemu ya tatu.
Anasema mtume muhammad (s.a.w) الحياء والإيمان قرناء
جميعا، فإذا رفع أحدهما رفع الآخر
"Haya na imani ni vitu vyenye kwenda sambamba kwa mwanadamu, na k**a kitaondoshwa kimoja wapo basi na kingine hakitobakia."
IMANI ni kiunganishi kitukufu kati ya mja na mola wake, na ktk kuthibiti kwake au alama za kiunganishi hiki kwanza kabisa ni kutakasika nafsi ya mja, kuwa safi tabia zake ktk jamii na kuwa mazuri matendo yake, na haliwezi patikana mambo hayo ispokuwa itakapozalika ktk nafsi unyenyekevu ulio hai, unaoweza kuondosha maovu na kuhisi uzito kuyakimbilia mambo machafu.
Ama mtu kung'ang'ania mambo yaliyo na udhalili bila ya kuyafanya kuwa ndio ibada kwake, na kujitosa ktk madhambi madogo madogo madogo bila kukusudia kuyafanya, hilo nalo linaashiria upungufu wa HAYA kwa mja, kisha upungufu wa IMANI YAKE.
Na dalili ya hilo ni kwamba kila anapopoteza mtu HAYA , basi atakuwa anapanda kidogo kidogo kutoka ktk ubaya mpk ubaya zaidi, na ataporomoka ktk tabia dhalili mpk tabia dhalili zaidi, hatoacha kuwa anaanguka mpk ktk darja ya mwisho ya udhalili na huo ni mwisho mbaya kwa mwanadamu.
ALLAH atuepushe na mtihani huo na atujaalie mwisho mwema. Aaaamin.....!!!
insha ALLAH tutaendelea......!!!!!!!!